Kanda Namba Tatu yajifagilia utoaji huduma bora kwa mteja
Na. mwandishi Wetu, KIZOTA
Kanda Namba Tatu katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma
inaadhimisha Wiki ya Huduma kwa Mteja kwa kuhakikisha huduma muhimu kwa
wananchi na wafanyabiashara zinapatikana muda wote na kwa wakati.
Huduma muhimu zinazotolewa ni pamoja na ukataji wa leseni ya biashara, malipo ya ushuru, malipo ya kodi za majengo, huduma ya elimu ya msingi na sekondari, huduma za ustawi wa jamii, usajili wa vikundi na asasi za kiraia, vibali vya ujenzi, vibali vya sherehe, upatikanaji wa hati na ushuru wa mabango.
Meneja wa Kanda Namba Tatu, Fanuel Lawrence, alisema kuwa
muitikio wa wananchi ni mkubwa na umeonesha dhamira ya wazi ya wananchi kupata
huduma stahiki. “Wiki ya Huduma kwa Mteja ni muhimu sana kwetu, inatuonesha
namna tunavyowahudumia wananchi na mapokeo ya huduma walizopata. Pia inatupa
mwanga wa kuboresha zaidi huduma zetu. Kwa ujumla tunafanya kazi kwa weledi na
kwa kuzingatia utaratibu lakini katika yote hayo tunatanguliza huduma bora kwa
wateja wetu” alisema Lawrence.
Nae, Afisa Biashara katika Halmashauri ya Jiji la
Dodoma, Steven Maufi, alisema kuwa maadhimisho hayo ni ukumbusho kwa watumishi
kutoa huduma bora na kujenga mahusiano mazuri na wananchi. “Huduma nzuri huleta
furaha na mshikamano. Niwahimize watumishi wenzangu kuzingatia lugha za staha,
kusikiliza kwa makini wateja na kutoa maamuzi yenye busara kwa mustakabali wa
pande zote mbili yaani kwa mteja na halmashauri” alisema.
Kwa upande wake mkazi wa Kata ya Kizota, James Wamalya
alieleza kuridhishwa na uwepo wa ofisi hizo karibu na maeneo yao. “Tunashukuru
sana ofisi hizi za kanda kuletwa karibu. Zimetusaidia kuokoa muda mwingi na
gharama za kufuata huduma mjini. Hongera kwa halmashauri kwa kutujali sisi
wananchi” alieleza.
Maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Mteja yanathibitisha
dhamira ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma katika kuhakikisha wananchi wanapata
huduma bora, haraka na kwa ukaribu.
MWISHO
Comments
Post a Comment