Jiji la Dodoma lajikita kuimarisha Mawasiliano na wananchi Wiki ya Huduma kwa Mteja
Na. Leah Mabalwe, DODOMA
Halmashauri ya Jiji la Dodoma inatumia maadhimisho ya
Wiki ya Huduma kwa Mteja kutathmini mfumo wa utoaji huduma kwa wananchi na
kuhamasisha mawasiliano bora ili kuwaweka wananchi karibu zaidi na halmashauri
yao.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Dennis Gondwe akifafanua jambo
Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano
Serikalini, Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dennis Gondwe, alipokuwa akijibu
swali la jinsi halmashauri inavyotumia maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Mteja
ofisini kwake.
Gondwe alisema kuwa Wiki ya Huduma kwa Mteja ni wiki
inayoikumbusha halmashauri kuwa ipo kwa ajili ya utoaji huduma kwa wananchi.
“Msingi wa uwepo wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma ni utoaji wa huduma bora na
za viwango kwa wananchi. Ni kipindi ambacho tunatafakari hali ya huduma
tunayotoa kwa wananchi, ni kipindi ambacho tunatafakari kule tunapolenga kufika
katika viwango vya utoaji wa huduma. Menejimenti ya halmashauri inalenga kufika
sehemu ambapo malalamiko ya huduma zinazotolewa kwa wananchi inakuwa ni
historia. Tunataka kufika sehemu ambapo mwananchi hakumbuki mara ya mwisho
ilikuwa lini kupata huduma chini ya kiwango, mara ya mwisho lini kupanga foleni
kusubiri huduma” alisema Gondwe.
Menejimenti ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma
imeanzisha mfumo wa utoaji huduma kupitia kanda. “Jumla ya kanda saba za utoaji
huduma zimeundwa kwa lengo la kuwasogezea huduma wananchi karibu na maeneo
waliyopo. Halmashauri imewafuata wananchi walipo, hivyo, tunaongelea huduma
karibu na wananchi, tunaongelea huduma ndani ya muda mfupi, tunaongelea huduma
bila kutumia gharama na muda kuifuata, hii ndiyo Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Tunatumia wiki hii ya huduma kwa mteja, kuboresha zaidi mawasiliano yetu na
wananchi ambao tunawahudumia, kwa kuwasikiliza, kushauriana nao na kupata
mrejesho wa huduma tunazotoa ili tuendelee kuwa bora zaidi. Maadhimisho haya yanafanyika
hapa ofisi kuu na katika ofisi zetu zote za kanda” alisisitiza Gondwe.
Katika
hatua nyingine, mkazi wa Kata ya Iyumbu, Lucas Moses alieleza kuwa mfumo wa
utoaji huduma kupitia kanda umeboresha upatikanaji wa huduma kwa wananchi,
kwasababu wanahudumiwa karibu na makazi yao jambo lililopunguza muda na
gharama. “Kupitia mfumo wa kanda, tunapata huduma karibu na haraka zaidi.
Tunashauri maboresho zaidi kwenye miundombinu” alisema Moses.
Kwa
upande wake, mfanyabiashara Edmund Mngassa aliyeenda kupata huduma katika Ofisi
ya Kanda Namba Moja, alipongeza huduma bora aliyopata katika Kanda Namba Moja,
akisema kuwa zimekuwa chachu ya mabadiliko katika safari yake ya kibiashara.
“Sikuwahi kufikiria kuwa ningeweza kupata huduma nyingi kiasi hiki sehemu moja
na ndani ya muda mfupi. Zaidi ya yote nimepokelewa vizuri, lakini pia kuna
baadhi ya vitu ambavyo nilikuwa sina uelewa navyo maafisa wameweza
kunielewesha. Hivyo, niwasisitize wafanyabiashara wenzangu tusikae nyuma, tuje
kukata leseni za biashara na huduma zingine ili tuweze kufanya biashara kwa
uhalali’’ alisema Mngassa.
Comments
Post a Comment