Kanda Namba Mbili yang'ara kwa huduma bora kwa wateja

Na. Tutindaga Nkwindi DODOMA

Kanda Namba Mbili imeendelea kungara kwa kutoa huduma bora zenye tija kwa wananchi katika maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Mteja yanayoendelea katika ofisi ya kanda kwa kushirikisha watumishi pamoja na wananchi kutoka maeneo mengi ya kata zinazounda kanda hiyo.



Maadhimisho hayo ni ukumbusho wa kuimarisha mawasiliano kati ya watumishi na wananchi, sambamba na kujadili changamoto na mafanikio katika utoaji wa huduma kwa umma.

 Meneja wa Kanda Namba Mbili, Abeid Msangi alisema kuwa utoaji wa huduma bora ni wajibu wa kila mtumishi wa umma na njia sahihi ya kujenga uaminifu wa wananchi kwa taasisi za serikali. Huduma bora kwa wateja ni moyo wa utendaji. Tunapaswa kuwa wabunifu, wakarimu na kujituma ili kila mwananchi ajisikie kuthaminiwa anapohudumiwa alisema Msangi.

Kwa upande wake, Afisa Biashara wa Kanda Namba Mbili, Ruth Kingu alisema kuwa Wiki ya Huduma kwa Mteja ni fursa muhimu ya kupokea mrejesho kutoka kwa wananchi na kuboresha zaidi mifumo ya utoaji huduma. “Tunajifunza mengi kupitia maoni ya wateja. Lengo letu ni kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma bora, haraka na kwa ufanisi alisema Kingu.

 Mfanyabiashara kutoka Kata ya Nzuguni, Theresia John aliipongeza kanda hiyo kwa huduma nzuri wanazotoa na utayari wa watumishi kuwahudumia wananchi kwa weledi na kwa wakati. Tumeona mabadiliko makubwa, huduma zinapatikana kwa urahisi na watumishi wanatupokea vizuri. Hongera kwa timu nzima ya Kanda Namba Mbili kwa kazi nzuri alisema John.

 


Katika hatua nyingine, mkazi wa Kata ya Iyumbu, Lucas Moses alieleza kuwa mfumo wa utoaji huduma kupitia kanda umeboresha upatikanaji wa huduma kwa wananchi, kwasababu wanahudumiwa karibu na makazi yao jambo lililopunguza muda na gharama. Kupitia mfumo wa kanda, tunapata huduma karibu na haraka zaidi. Tunashauri maboresho zaidi kwenye miundombinu alisema Moses.

 Maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Mteja yanawakumbusha watumishi wote kuendeleza ubunifu, uwajibikaji na uwazi katika utendaji wao ili kuimarisha uhusiano mzuri kati ya serikali na wananchi na kuendeleza dhana ya utoaji huduma bora kwa wote.

 

Comments

Popular Posts

Kanda Namba Mbili yaendelea kutoa huduma bora kwa wananchi

JIJI LA DODOMA KUPELEKA MIL 50 ZAHANATI YA KIKUYU