Kanda Namba Mbili yaendelea kutoa huduma bora kwa wananchi
Na. Tutindaga Nkwindi, NZUGUNI
Kanda Namba Mbili inayohudumia kata tano za Nzuguni, Ipagala,
Ihumwa, Mtumba na Kikombo imeendelea kutoa huduma bora kwa wananchi, ikiwa ni
sehemu ya mkakati wa kuhakikisha kila mkazi wa kanda hiyo anapata huduma kwa
wakati na kwa kiwango kinachostahili.
Akizungumza na waandishi wa habari Meneja wa Kanda hiyo, Abeid Msangi alisema kuwa kanda imejipanga vizuri katika kusimamia utoaji wa huduma kwa kuzingatia maadili ya utumishi wa umma, ubunifu na uwajibikaji.
“Tunaendelea kuhakikisha wananchi
wanapata huduma kwa haraka na kwa ubora. Tumeweka mifumo ya ufuatiliaji wa
maombi ya wananchi na kuboresha mawasiliano kati ya ofisi na jamii ili kuongeza
ufanisi” alisema Msangi.
Aidha, alieleza kuwa maafisa walioko katika kanda hiyo
wamekuwa wakipatiwa mafunzo ya mara kwa mara kuhusu utoaji wa huduma kwa wateja
na matumizi ya teknolojia katika kushughulikia maombi ya wananchi, hatua ambayo
imepunguza changamoto za ucheleweshaji wa huduma.
Vilevile, alisisitiza kuwa ubunifu na uwajibikaji ndiyo nguzo kuu zinazoiongoza kanda hiyo katika kutoa huduma bora, huku akiwataka watumishi kuendelea kujituma kwa bidii ili kufikia matarajio ya wananchi.
Kwa upande wake Anna James, mkazi wa Kata ya Ipagala
aliipongeza Kanda Namba Mbili kwa huduma zake bora na upokeaji mzuri kwa
wananchi wanaofika kupata huduma.
“Nimekuwa nikifika ofisini mara
kadhaa, na kwa kweli huduma zimeboreshwa sana. Watumishi wanatupokea vizuri,
wanatoa maelezo kwa heshima na wanashughulikia changamoto zetu kwa wakati” alisema James.
Kanda Namba Mbili imeendelea kuwa mfano wa kuigwa katika
utoaji wa huduma bora kwa wananchi, ikiakisi dhamira ya Halmashauri ya Jiji la
Dodoma ya kujenga utamaduni wa uwajibikaji, ubunifu na huduma zenye ubora kwa
jamii.
Comments
Post a Comment