Mkataba ujenzi Uwanja wa Mpira wa Miguu wasainiwa Dodoma
Na. Aisha Ibrahim, DODOMA
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni,
Sanaa na Michezo, Greyson Msigwa, amesema mradi wa ujenzi wa uwanja wa mpira wa
miguu Dodoma, utakaoweza kubeba watu 32,000 ambao utagharimu kiasi cha shilingi
bilioni 352 fedha za kitanzania, unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 24,
chini ya serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Aliyasema hayo katika hafla ya utiaji saini
mkataba wa ujenzi wa uwanja wa mpira wa miguu Dodoma, uliohusisha wizara hiyo
na Kampuni ya Lemonta SPA, iliofanyika kiwanja cha Changamani, Kata ya Nzuguni,
jijini Dodoma.
Akizungumza kuhusu lengo la ujenzi wa uwanja
huo, Msigwa alisema, mradi huo ni fursa kwa maendeleo ya michezo kwa wakazi wa
Jiji la Dodoma kwasababu uwanja huo utatumika katika mashindano mbalimbali
kitaifa na kimataifa ili kuhakikisha sekta ya michezo inazidi kukua.
“Mradi huu ni fursa kwa maendeleo ya wakazi
wa Dodoma lakini ni fursa kubwa kwa wanamichezo katika kukuza vipaji vyao, na
sisi kama wizara tumejipanga ili uwanja huu utumike kwa mashindano mbalimbali
ya kitaifa na kimataifa” alisema Msigwa.
Aidha, aliahidi kuwa atahakikisha wanasimamia
mradi huo kwa umakini wa hali ya juu mpaka pale utakapo kamilika ikiwa ni
kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia
Suluhu Hassan.
“Mheshimiwa waziri, naomba kutoa ahadi mbele
yako na mbele ya watanzania, sisi watendaji wako tutasimamia mradi huu hatua
kwa hatua, kucha kwa kucha mpaka ukamilike” alisema Msigwa.
Pia, aliipongeza serikali ya awamu ya sita chini
ya utawala wa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa juhudi na kazi nzuri inayoendelea
kufanyika kwa kuhakikisha mradi huo unashughulikiwa ipasavyo mpaka kukamilika.
Nae, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary
Senyamule, alisema kuwa Dodoma inajivunia kuwa na vivutio vingi vya utalii
ikiwa ni pamoja na utalii wa michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu ambapo
ilikuwa ni ndoto ya muda mrefu ya wakazi wa maeneo yote ya Jiji la Dodoma kuwa
na uwanja mzuri wenye viwango vya hali ya juu.
“Moja ya kipaumbele ni Dodoma kuwa mkoa wa
utalii na utalii huo ni pamoja na michezo ya mpira wa miguu na tunaishi kwa
imani kuwa uwanja huo utakamilika hivyo tujipange kuwa utalii wa michezo
utakuwa ni tija kwa wananchi wa Mkoa wa Dodoma” alisema Senyamule.
Sambamba na hayo, aliongeza kuwa matarajio ya
kila mkazi wa Jiji la Dodoma, ni kuona mechi za AFCON zakichezwa katika uwanja
huo ikiwa ni njia mojawapo ya kukuza sekta ya michezo kitaifa na kimataifa.
“Tumekuwa tukisema kwa wananchi kuwa Dodoma,
AFCON itachezwa iwe kwa mechi au kwa mazoezi lakini tunatamani matone ya AFCON
yatudondokee hapa Dodoma na ndio maana wananchi kila siku wakawa wanasema hivi
kweli!! uwanja upo? Yaani wanaanza kuona kama AFCON haitowahusu” alisema
Senyamule.
Alimaliza kwa kusema kuwa wakazi wa Dodoma
wapo tayari kushirikiana na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ili
kuhakikisha ujenzi wa mradi huo unatimia kwa wakati maalum uliopangwa.
MWISHO
Comments
Post a Comment