Wanawake Jiji la Dodoma washauriwa kuandaa vyakula kwa nishati safi ya kupikia
Na. Faraja Mbise, DODOMA
Wanawake
wameshauriwa kutumia nishati safi ya kupikia katika kuandaa vyakula vya watoto kwasababu
upatikanaji wake ni rahisi ukilinganisha na matumizi ya nishati chafu ya
kupikia kama vile mkaa na kuni kutokana na kuwa inaokoa muda na ni salama kwa
mazingira.
Afisa Lishe wa Kituo cha Afya cha Makole, Frida Mollel wakati akitoa mafunzo kwa vitendo juu ya jiko darasa kwa akina mama wanaonyonyesha waliohudhuria kliniki
Ushauri
huo ulitolewa na Afisa Lishe wa Kituo cha Afya cha Makole, Frida Mollel wakati
akiwafundisha juu ya jiko darasa kwa akina mama wanaonyonyesha waliohudhuria kliniki
katika Kituo cha Afya Makole kilichopo Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Mollel
aliwataka kutumia nishati safi ya kupikia wanapoandaa chakula cha watoto wao
kwasababu upatikanaji wake ni rahisi na usalama kwa mtoto ni mkubwa zaidi
ukilinganisha na matumizi ya nishati chafu ya kupikia. “Sambamba na elimu ambayo
tumeitoa, utumiaji wa nishati safi umekuwa ukirahisisha uandaaji wa vyakula,
ambayo inatoa usalama wa mtoto. Kwa mfano, mama ambaye atapika kwa kutumia gesi,
uji wake ataweza kuusimamia na kusubiri kwasababu ule uji utaiva kwa haraka
lakini kwa mama ambaye anatumia mkaa, itabidi atumie kwa muda mrefu, muda
mwingine anaweza kujisahau na mtoto akaungua. Lakini pia tumeona matukio ya watoto
kuungua kwa moto yamepungua kwasababu ya nishati safi” alisema Mollel.
Akiongelea
uandaaji wa chakula, alisema kuwa ni muhimu kuzingatia makundi yote ya chakula
na kuachana na mfumo uliopo wa kuandaa kundi moja tu la chakula. “Tamaduni zetu
za kiafrika tumekuwa tukiandaa aina moja ya chakula kwa watoto, ambayo
tukiangalia kwenye taarifa ya Digital Health Incentive Scheme (DHIS) inaonesha
kwamba tuna ‘low food diversification’ kwa watoto ambayo inatupelekea
kwa ‘indicator’ hiyo kuwa chini sana. Kwahiyo, mafunzo haya ya jiko
darasa yameweza kuwasaidia akina mama kutumia makundi mengi ya vyakula kwa
wakati mmoja na kuhama kutoka kutumia kundi moja la wanga kwa wingi kwenye
vyakula kama kutumia aina ya mizizi na wanga. Kinamama kama mnavyojua walikuwa
na kawaida ya kuandaa unga wa lishe ambapo wanaweka mahindi, mchele na vitu
vingine ambavyo si afya nzuri kwa watoto kwasababu havitoi virutubisho
vinavyohitajika kwa watoto” alisisitiza Mollel.
Kwa
upande wake, mtoa huduma ya unyonyeshaji sahihi kwa watoto wachanga katika Kituo
cha Afya Makole, Sylivia Kitalo alitoa ushauri kuhusu umuhimu wa kutumia
nishati safi ya kupikia, namna inavyowasaidia akina mama wanaonyonyesha na
kutaja madhara ya kutumia nishati chafu ya kupikia kama mkaa na kuni. “Nishati
safi ya kupikia ni nzuri na tunamshukuru Rais wa nchi yetu, Mama Samia Suluhu
Hassan kwa kutuletea nishati safi ya kupikia, zinaweka mji safi, miti inakuwa
ya kutosha kama haijakatwa. Ninawashauri kina mama ambao bado wanatumia nishati
chafu ya kupikia, ninawaomba waepukane nayo na waanze kutumia nishati safi ya kupikia
ambayo ni umeme na gasi” alisema Kitalo.
Nae
mnufaika wa elimu ya jiko darasa, Esther Samwel alielezea namna ambavyo elimu
kupitia jiko darasa ilivyomsaidia kuandaa lishe bora na alielezea umuhimu wa
kutumia nishati safi ya kupikia na usalama wake kwa mazingira ya mtoto. “Nimekutana
na darasa zuri ambalo limenisaidia kuelewa kwa baadhi ya vitu na pia
nimejifunza namna ya kuandaa vyakula kwa ajili ya watoto, hata sisi wajawazito na
kutengeneza lishe bora kwa ajili ya watoto wetu. Tumejifunza kutumia nishati
bora ya kupikia. Sio lazima tutumie mikaa au kuni kwasababu inaharibu hali ya
hewa. Kwahiyo, ni vizuri akina mama majumbani tujitahidi kutumia nishati bora
na inatusaidia kuwahi kupika kwa haraka” alieleza Samwel.
Vilevile,
mkazi wa Mtaa wa Ihumwa, Zena Selemani alitoa faida za kutumia nishati safi ya
kupikia jinsi zinavyoweka mazingira mazuri kwa mtoto ili asidhurike na moto na
namna ambavyo inawapa fursa katika kufanya shughuli nyingine za maendeleo. “Gesi
inanisaidia kupika chakula chochote kwa wakati hasa chakula cha mtoto, maana
muda mwingine mtoto anaweza akawa anasumbua lakini ukienda kupika kwenye gasi
unapika chakula chake kwa wakati na anakula kwa wakati. Kutumia nishati safi ya
kupikia inanipa muda wa kutosha wa kuandaa chakula cha mtoto na cha familia. Kutumia
nishati ya kupikia ya gesi au umeme, kiukweli chakula cha mtoto kinakuwa katika
mazingira salama kwasababu hakuna zile athari za kurukiwa na moto maana muda
mwingine mkaa unatoa moshi. Kwahiyo, ukitumia gesi, hizo athari zinakuwa
hazipo” alisema Selemani.
MWISHO
Comments
Post a Comment