Mwenge wa Uhuru 2024 waweka jiwe la msingi Kituo cha vyombo vya habari cha Dodoma Media Group
Na. Dennis Gondwe, MIYUJI
KIONGOZI wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa mwaka 2024
Godfrey Mnzava ameweka jiwe la msingi na kupongeza uwekezaji uliofanywa na Dodoma
Media Group baada ya kutembelea na kukagua kituo cha vyombo vya habari cha
Dodoma Media Group kilichojengwa eneo la Miyuji.
Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa mwaka 2024 Godfrey Mnzava baada ya kuweka jiwe la msingi kituo cha vyombo vya habari Dodoma Media Group
Mnzava baada ya kutembelea, kukagua na kujiridhisha na
uwekezaji huo alipongeza na kusema kuwa ni uwekezaji mkubwa na mzuri. Alisema kuwa
serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan
imeweka mazingira mazuri kwa uwekezaji wa sekta binafsi nchini. Mazingira ya
ufanyaji kazi kwa vyombo binafsi vya habari yameboreshwa katika kipindi chake, aliongeza.
Aidha, aliweka jiwe la msingi mradi wa kituo cha vyombo vya Habari cha Dodoma Media
Group.
Akiongelea
gharama za mradi huo, meneja mkuu, Zania Miraji alisema kuwa hadi kukamilika
utagharimu shilingi 1,000,000,000. Alisema kuwa hatua iliyofikiwa kiasi cha
shilingi 700,000,000 kimetumika sawa na asilimia 70, akivitaja vyanzo vya fedha
kuwa ni matangazo ya biashara, mkopo na mapato binafsi ya mkurugenzi.
Mradi wa kituo cha vyombo vya habari cha Dodoma Media Group
ulianza kutekelezwa tarehe 1 Oktoba, 2018 ukitarajiwa kukamilika tarehe 31
Desemba, 2024, ukihusisha ujenzi wa majengo ya studio za redio, televisheni,
samani na mifumo ya umeme na maji.
MWISHO
Comments
Post a Comment