Mtendaji Kata Nkuhungu anena fursa kongamano la vijana
Na. Dennis Gondwe, NKUHUNGU
Kongamano la vijana ni fursa ya kuwakutanisha vijana
wa Kata ya Nkuhungu na wenzao kutoka maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Dodoma kujadili
fursa zilizopo na jinsi ya kuzifikia kwa ajili ya kujiletea maendeleo.
Afisa Mtendaji wa Kata ya Nkuhungu, Mwasiti Migilla akiwa katika moja ya majukumu yake
Baadhi ya washiriki wa kongamano la vijana Wilaya ya Dodoma |
Kauli hiyo ilitolewa na Afisa Mtendaji wa Kata ya Nkuhungu, Mwasiti Migilla alipokuwa akiwapokea vijana wanaohuduria kongamano la
vijana linalofanyika katika uwanja wa Shule ya Msingi Nkuhungu jijini Dodoma
likienda sambamba na mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2024 wilayani Dodoma.
Migilla alisema kuwa kata yake imepata heshima ya
kuwa mwenyeji wa kongamano la vijana na mkesha wa Mwenge wa Uhuru mwaka 2024
katika Wilaya ya Dodoma. “Matukio haya mawili ni makubwa na ni heshima kubwa kwetu
wananchi wa Kata ya Nkuhungu. Vijana wanapata fursa ya kubadilishana mawazo na
uzoefu pamoja na kujadili fursa mbalimbali zilizopo katika wilaya yao kwa lengo
la kuzifikia na kujiletea maendeleo” alisema Migilla.
Akiongelea mkesha wa Mwenge wa Uhuru mwaka 2024,
alisema kuwa wananchi wa Kata ya Nkuhungu ni wafuasi wa Mwenge wa Uhuru tangu
miaka ya nyuma. “Kata ya Nkuhungu huwa tunakesha na Mwenge wa Uhuru, yaani huwa
hakuna kulala. Nitumie fursa hii kuwaalika wananchi wote wa Nkuhungu na maeneo
mengine ya Wilaya ya Dodoma kujitokeza kwa wingi kwenye mkesha. Kutakuwa na
burudani zinazogusa makundi yote hivyo, hii siyo ya kusimuliwa” Migilla.
Kwa upande wake mshiriki wa kongamano la vijana,
Msifuni Mwasi alisema kuwa kongamano hilo ni muhimu kwa sababu linawakutanisha
vijana wengi kwa pamoja ili kuweza kujadili fursa na changamoto zao. Aidha,
alishauri makongamano kama hayo yawe yanafanyika mara kwa mara yakigusa na vijana
wa maeneo ya pembezoni.
MWISHO
Comments
Post a Comment