Dodoma English Medium imewasaidia wazazi wa kipato cha kati kusomesha
Na. Dennis Gondwe, IPAGALA
MRADI wa ujenzi wa Shule ya Awali na Msingi Dodoma
English Medium umewasaidia wazazi wenye kipato cha kati kusomesha watoto wao
katika shule ya mchepuo wa kiingereza karibu na maeneo yao kwa gharama nafuu.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Divisheni ya Elimu ya Awali
na Msingi Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Prisca Myalla alipokuwa akisoma
taarifa ya mradi wa ujenzi wa Shule ya Awali na Msingi ya Dodoma English Medium
kwa Kiogozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa mwaka 2024.
Akiongelea faida za mradi huo alizitaja kuwa ni kuwasaidia wazazi wenye kipato cha kati kupata
fursa ya kusomesha watoto kwenye shule ya mchepuo wa kiingereza. Faida nyingine aliitaja kuwa ni wananchi
kusogezewa huduma ya shule karibu ambapo watoto walikuwa wanasafiri umbali
mrefu kufuata huduma ya elimu pia wanafunzi wanapata elimu bora kwa gharama
nafuu ukilinganisha na shule binafsi. “Ndugu Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2024, mradi
umelenga kutoa elimu bora ambayo itasaidia kupata wataalamu mbalimbali kwa
maendeleo ya uchumi kwa Taifa letu, kuboresha mazingira ya kujifunzia na
kufundishia, kuongeza
uandikishaji wa wanafunzi wa darasa la awali na msingi na kuwezesha wananchi wenye
kipato cha kati kuwapeleka watoto katika shule za mchepuo wa kiingereza” alisema Myalla.
Akiongelea
gharama za mradi alisema kuwa utekelezaji wa mradi huo ulianza tarehe 05 Mei, 2023
na kukamilika tarehe 30 Desemba, 2023 kwa gharama ya shilingi 458,047,800.00.
“Ndugu Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2024, shule
hii iliwekewa jiwe la msingi na Abdalla Shaib Kaimu Kiongozi wa Mbio za
Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2023 tarehe 03 Oktoba, 2023. Pia
tunatoa shukrani za dhati kwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, kwa kuendelea kuboresha sekta ya elimu
kwa kuimarisha miundombinu ya
kujifunzia na kufundishia. Halmashauri ya Jiji la Dodoma inaahidi kutunza miundombinu ya shule hii” alisema Myalla.
Shule ya Awali
na Msingi Dodoma English Medium yenye usajili namba EM 20048, ipo Kata ya
Ipagala, Mtaa wa Swaswa yenye ukubwa wa eneo la mita za mraba 35,400 ikiwa na jumla ya wanafunzi 270 wavulana 147 na wasichana
123 na walimu 14. Shule inatekeleza jumbe za Mwenge wa
Uhuru 2024 kwa vitendo, kupitia ujumbe wa “Tunza Mazingira na Shiriki Uchaguzi
wa Serikali za Mitaa kwa ujenzi wa
Taifa endelevu” ambapo shule imepanda miti 446 kati ya hiyo miti 279 ni ya
matunda na miti 167 kwa ajili ya kivuli.
MWISHO
Comments
Post a Comment