Mwenge wa Uhuru 2024 kutembelea miradi ya Bil. 7 Wilaya ya Dodoma
Na. Dennis Gondwe, DODOMA
MWENGE wa Uhuru mwaka 2024 utatembelea, kuzindua na
kuweka jiwe la msingi jumla ya miradi saba yenye thamani ya shilingi 7,096,668,714.32
wilayani Dodoma.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma,
Alhaj Jabir Shekimweri alipokuwa akipokea Mwenge wa Uhuru kutoka kwa Mkuu wa Wilaya
ya Chemba, Gerald Mongela mapema leo katika uwanja wa michezo wa Shule ya Sekondari
John Merlin iliyopo Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Alhaj Shekimweri alisema “ninakiri kwa dhati ya moyo
wangu kuupokea Mwenge wa Uhuru kutoka kwako Mkuu wa Wilaya ya Chemba, Gerald
Mongela. Aidha, ninakiri kumpokea Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa ndugu
Godfrey Mnzava pamoja na wenzake watano. Mwenge wa Uhuru ukiwa wilayani Dodoma
utatembelea miradi saba yenye jumla ya shilingi 7,096,668,714.32. Vilevile, Mwenge wa Uhuru utapata nafasi ya kusalimia kongamano
la vijana. Nikuhakikishie kwamba Mwenge wa Uhuru katika Wilaya ya Dodoma tutautendea
haki kwa kukimbia nao kama ratiba ilivyopangwa”.
Awali akikabidhi Mwenge wa Uhuru, Mkuu wa Wilaya ya Chemba,
Gerald Mongela alisema “nakukabidhi Mwenge wa Uhuru Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir
Shekimweri, Mwenge huu ukiwa unawake, unameremeta na unapendeza sana. Aidha,
ninakukabidhi na itifaki ya wakimbiza Mwenge wa Uhuru kitaifa sita wakiwa na
afya njema wakiongozwa na Godfrey Mnzava”.
Alisema kuwa Mwenge wa Uhuru ukiwa ndani ya Wilaya ya chemba,
ulikimbizwa bila kusimama umbali wa kilometa 163 ukitembelea, kukagua na kuweka
jiwe la msingi kwenye miradi sita yenye thamani ya shilingi 1,293,815,620. Mwenge
wa Uhuru katika Wilaya ya Chemba umeacha alama kubwa, aliongeza.
Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, John Kayombo akiendelea na itifaki ya Mwenge wa Uhuru mwaka 2024
Diwani wa Kata ya Chamwino, Jumanne Ngede akiendelea na itifaki ya Mwenge wa Uhuru mwaka 2024 Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma, Prof. Davis Mwamfupe akiendelea na itifaki ya Mwenge wa Uhuru mwaka 2024
MWISHO
Comments
Post a Comment