Msalato Sekondari wamshukuru Rais, Dkt. Samia ujenzi wa mabweni
Na. Dennis Gondwe, MSALATO
SHULE ya Sekondari ya Wasichana Msalato inamshukuru Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha
nyingi za ujenzi wa miundombinu na kuwatengenezea mazingira bora ya kufundishia
na kujifunzia wanafunzi kwa lengo la kukuza viwango vya taaluma nchini.
Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Wasichana, Msalato, Mwl. Mwasiti Msokola alipokuwa akiongelea juhudi za serikali katika ujenzi wa miundombinu |
Shukrani hizo zilitolewa na Mkuu wa Shule ya
Sekondari ya Wasichana, Msalato, Mwl. Mwasiti Msokola alipokuwa akiongelea
juhudi za serikali katika ujenzi wa miundombinu mbele ya ugeni kutoka Wizara ya
Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar uliotembelea shule hiyo.
“Tunamshukuru sana Rais, Dkt. Samia Suluhu
Hassan kwa upande wa elimu Shule ya Sekondari ya wasichana Msalato ametuona kwa
sababu mwaka jana ametuletea fedha shilingi 428,000,000 kutuwezesha kujenga
mabweni mawili ya maadalizi ya kupokea wanafunzi wa kidato cha tano. Vilevile, tukapewa
vyumba saba vya madarasa na matundu 10 ya vyoo. Haikutosha tukapewa tena shilingi
260,000,000 kwa ajili ya kujenga mabweni mengine mawili. Kukamilika kwa
miundombinu hiyo kumepunguza msongamano wa wanafunzi darasani na katika mabweni
kila mwanafunzi ana kitanda chake. Tunamshukuru sana rais wetu” alisema Mwl.
Msokola kwa sauti ya shukrani.
Wakati huohuo, Mkuu wa Divisheni ya Elimu ya Sekondari
Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Mwl. Zainab Abdallah alisema kuwa motisha kwa
walimu imesaidia kuinua hali ya taaluma. “Motisha ni kila
kitu katika elimu kama hakuna motisha ni kazi ngumu sana. Tarehe 17 Februari,
2024 tulifanya kikao cha wadau wa elimu pamoja na utoaji tuzo kwa walimu
waliofanya vizuri katika masomo yao ili tujadiliane jinsi ya kuboresha elimu. Halmashauri
tuliipatia shule hii tuzo na tuna utaratibu wa kununua alama ‘A’ kwa kila
mwalimu anayezalisha ‘A’ tunailipa shilingi 10,000. Kwa hiyo hapa walinimalizia
kibubu changu hapa Msalato. Hapa kulikuwa na mwalimu ana ‘A’ 86 za Kiswahili, mwalimu
ana ‘A’ 78 Baiolojia na mwalimu ana ‘A’ 74 za Kemia na wote tuliwazawadia”
alisema Mwl. Zainab.
Mkuu wa Divisheni ya Elimu ya Sekondari Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Mwl. Zainab Abdallah akifuatilia majaribio katika Maabara ya Kemia |
Wakiwa
shuleni hapo, timu ya wageni kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar
walielezwa usimamiaji wa nidhamu ya walimu na wanafunzi, jitihada za shule
kumaliza mada kwa wakati na wanafunzi kufanya majaribio ya sayansi kwa vitendo.
MWISHO
Comments
Post a Comment