Tamisemi yajivumia taaluma Bunge Sekondari
Na. Dennis Gondwe, DODOMA
OFISI
ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa inajivunia maendeleo ya kitaaluma
katika Shule ya Sekondari ya wasichana Bunge kufuatia uwekezaji waliofanya na
serikali shuleni hapo.
Mkurugenzi Msaidizi wa Elimu Ofisi ya Rais, Tamisemi, Mwl. Ernest Hinju (katikati) akisisitiza jambo |
Kauli
hiyo ilitolewa na Mkurugenzi Msaidizi wa Elimu Ofisi ya Rais, Tamisemi, Mwl. Ernest
Hinju alipoongoza ujumbe kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar kutembelea
shule hiyo.
Mwl.
Hinju alisema “leo tulikuwa katika ziara ya kuwakaribisha na kuwatembeza wageni
wetu kutoka Zanzibar ambao ni Mkurugenzi wa Elimu Maandalizi na Msingi na Mkurugenzi
wa Elimu ya Sekondari pamoja na wasaidizi wao. Lengo ni kuja kujifunza kwa
pande mbili jinsi wanavyoendesha elimu. Katika shule ya sekondari ya wasichana
Bunge pamoja na mambo mengine tumeweza kuongea na wanafunzi na tumewakuta
wanafunzi wanapendeza na wanahari ya kujifunza. Shule ya Sekondari ya wasichana
Bunge imejengwa kwa hisani ya wabunge wa Tanzania na imethibitika jitihada ya Rais,
Dkt. Samia Suluhu Hassan alivyoweza kuongeza majengo mengine mengi kwa haraka.
Leo shule ina wanafunzi wa kidato cha tano na sita; na tumeshuhudia matokeo
yanapanda kwa kasi na walimu wanajituma sana. Tumetembelea maabara na wanafunzi
wanaweza kuonesha kazi wanazofanya vizuri sana.
Akisoma
taarifa ya shule, Mkuu wa Shule hiyo, Mwl. Salome Mkombola alisema kuwa shule
yake ina mikakati ya kukuza taaluma. “Mikakati hiyo ni kuzingatia ratiba ya
vipindi vyote kufundishwa. Pia tumekuwa na mitihani ya mara kwa mara
inayosahihishwa na kufanyiwa tathimini. Mkakati mwingine tumekuwa tukiwatambua
na kuwasaidia wanafunzi ambao hawafanyi vizuri kwenye mitihani yao na kuendesha
madarasa rekebishi pamoja na kutumia vipindi vya ziada ili kumaliza mihtasari
mapema na kupata muda mzuri wa kufanya mapitio ya maeneo ambayo yamekuwa
yakiwatatiza wanafunzi” alisema Mwl. Mkombola.
Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Bunge, Mwl. Salome Mkombola akisoma mikakati ya kukuza taaluma |
Akiongelea
kupanda kwa taaluma, mwalimu wa taaluma msaidizi, Mwl. Stephano Chipuza alisema
kuwa taaluma imekuwa ikipanda kila mwaka. “Kidato cha sita awamu ya kwanza
tulikuwa na Daraja la kwanza wanafunzi 17, daraja na pili wanafunzi 92 na
daraja la tatu wanafunzi 38. Hatukuwa na daraja la nne wala sifuri. GPA ile
hatukuridhika nayo. Mwaka jana daraja la kwanza walikuwa wanafunzi 54 maana
yake walipanda kutoka wanafunzi 17 mapaka 54. Daraja la pili wanafunzi 86 na daraja
la tatu wanafunzi 33. Hivyo, GPA ikawa inasogea kutoka 3.6 mpaka 2.8” alisema
Mwl. Chipuza.
Mwl. Stephano Chipuza, Mtaaluma msaidizi |
MWISHO
Comments
Post a Comment