Dodoma Sec kuongeza ufaulu kula mwaka
Na. Dennis Gondwe, DODOMA
SHULE
ya Sekondari Dodoma imekuwa ikiongeza ufaulu kila mwaka ikifikisha zaidi ya
asilimia 97 ya ufaulu wa jumla kutokana na ushirikiano uliopo baina ya wanafunzi,
uongozi wa shule na serikali.
![]() |
Mkuu wa Shule ya Sekondari Dodoma, Mwl. Francis Tumaini alipokuwa akielezea mwenendo wa shule yake katika ufaulu |
Kauli
hiyo ilitolewa na Mkuu wa Shule ya Sekondari Dodoma, Mwl. Francis Tumaini
alipokuwa akielezea mwenendo wa shule yake kwa wageni kutoka Wizara ya Elimu na
Mafunzo ya Amali wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar waliotembelea shule hiyo kwa
lengo la kujifunza.
Mwl.
Tumaini alisema “kwa hali ya ufaulu, tunaongeza ufaulu kila mwaka. Kwa mwaka
juzi ufaulu kwa daraja la kwanza hadi la tatu, lengo la serikali tufikie
asilimia 50. Sisi tulikuwa na asilimia 65. Mwaka jana tukawa na asilimia 67 na
mwaka huu tuna asilimia 68. Kwa ufaulu wa jumla kwa mwaka huu tuna asilimia zaidi
ya 97. Kwa matokeo ya kidato cha Nne, tulikuwa na wanafunzi 308 tuliowasajili,
waliofanya mtihani walikuwa 305. Walipata daraja la kwanza ni 41, daraja la
pili 101 na daraja la tatu 64. Hawa ukiwatafuta utakuta tupo asilimia 68 ambao
wanaweza kwenda vyuo na sekondari za juu. Hii inatuonesha tunapiga hatua ya
kitaaluma kwenda mbele”.
Akiongelea
matokeo ya kitaifa ya kidato cha sita kwa mwaka jana alisema kuwa shule yake
ilipata daraja la kwanza hadi la tatu pekee. “Hatukuwa na daraja la nne wala
sifuri. Ninawashukuru viongozi wetu wote kuanzia Ofisi ya Rais, Tamisemi, Wizara
ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma na Ofisi ya Mkurugenzi
wa Jiji hadi kwenye ofisi za kata tupo nao kwa karibu sana kuyafikia mafanikio
haya” alisema Mwl. Tumaini.
Alisema
kuwa shule yake imekuwa ikiwajengea uwezo viongozi wa serikali ya wanafunzi. “Tuna
serikali ya wanafunzi ambao tunawafundisha na kuwajenga kuwa viongozi wa imara
wa kesho. Kule wanaingia kwenye kamati mbalimbali zote zinaanza na walimu na zinashuka
hadi kwa wanafunzi. Lakini pia tuna bustani za mbogamboga kwa ajili ya kuwafundisha
wanafunzi umuhimu wa bustani hizo katika lishe bora kwao na kwa jamii
inayowazunguka” aliongeza Mwl. Tumaini.
MWISHO
Comments
Post a Comment