Afisa Elimu Jiji la Dodoma anunua jina la Rais Samia kwa Laki 5
Na. Dennis Gondwe, MIYUJI
MKUU
wa Divisheni ya Elimu Sekondari Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Zainab Abdallah
amefurahishwa na uwezo wa mwanafunzi mwenye mahitaji maalum, Angel Elias alipoandika
jina la Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutumia mdomo wake na kununua jina
hilo kwa shilingi 500,000.
Mwanafunzi Angel Elias wa shule ya Msingi Hombolo Bwawani anayeandika kwa kutumia mdomo |
Furaha
hiyo aliionesha katika kikao cha wadau wa elimu wa Halmashauri ya Jiji la
Dodoma kilichoambatana na utoaji tuzo za kitaaluma na kufanyika katika Shule ya
Msingi St. Gasper iliyopo Miyuji jijini hapa.
“Mheshimiwa
Mwenyekiti kabla ya yote, ninaomba kwa ridhaa yako kama hautajari, hilo neno
lililoandikwa na mtoto wangu Angel ‘I am so excited’. Nitalinunua kwa shilingi
500,000. Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya ya Dodoma ni ukweli kwamba hata wale
wanafunzi wasio na mahitaji maalum tunaowafundisha hawajifunzi haraka kama huyu
anavyo fanya” alisisitiza Mwl. Abdallah.
Akiunga
mkono tukio hilo, Mkuu wa Divisheni ya Elimu ya Awali na Msingi Halmashauri ya Jiji
la Dodoma, Mwl. Prisca Myalla alichangia shilingi 500,000. “Mheshimiwa
Mwenyekiti tunakwenda sambamba katika kuinua elimu kwa watoto wetu wenye
mahitaji maalum katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma” alisema Mwl. Myalla.
Wachangiaji
wengine katika kuunga mkono juhudi ni Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Dodoma iliyoahidi
kuchangia shilingi 500,000 na Afisa Elimu Taaluma kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa
Dodoma aliahidi kuchangia shilingi 200,000.
Kwa
upande wake, Mwl. Sarah Kapyela alimshukuru
Mungu kwa kuwawezesha wadau kusogeza mbele gurudumu la elimu kwa mazingira yaliyopo
katika kufundisha watoto wenye mahitaji maalum. “Watoto hawa tunawapa uangalifu
sana kutokana na hali zao. Mfano huyu mtoto (Angel) kuna kitanda chake na
godoro lake maalum, tunamuweka pale mbele anakuwa anaandika na tunamuelekeza ni
namna gani aweze kumudu masomo yake. Tunachomshukuru Mungu zaidi huyu mtoto
yupo darasa la tano amefaulu mtihani wake wa mwaka jana kuingia darasa la tano kwa
kupata wastani daraja ‘B’, tunamshukuru Mungu, na wadau wetu wa elimu na
serikali yetu kutusaidia kuinua hii elimu na kutupatia vifaa mbalimbali Mungu
azidi kuwaongezea na kuwatia nguvu pale mnapotoa” alisema Mwl. Kapyela.
Alisema
kuwa watoto wenye mahitaji maalum wanabidii sana darasani. “Hata wale wazazi
wanaowaficha watoto wao wenye ulemavu tunawaomba wawalete watoto kwenye hiki
kituo ambacho serikali imekitenga kwa ajili ya kuwahudumia. Na sisi tupo
tunajitoa kwa moyo zaidi kuweza kutekeleza hili jukumu Mungu aendelee kuwatia
nguvu nasisi kutukumbuka” alisema Mwl. Kapyela.
Mwl. Sarah Kapyela akuelezea umahili wa mwanafunzi Angel Elias darasani Mkuu wa Divisheni ya Elimu Sekondari Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Zainab Abdallah
MWISHO
Comments
Post a Comment