Wanafuzi Dodoma Sec watakiwa kusoma kwa bidii
Na. Dennis Gondwe, DODOMA
WANAFUNZI
wa Shule ya Sekondari Dodoma wametakiwa kusoma kwa bidii na kutumia mfumo wa
teknolojia ya ufundishaji mubashara kwa manufaa yao na vizazi vijavyo.
Mkurugenzi wa Idara ya Elimu Msingi na Maandalizi kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Fatma Ramadhani alipokuwa akiongea na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Dodoma |
Kauli
hiyo ilitolewa na Mkurugenzi wa Idara ya Elimu Msingi na Maandalizi kutoka Wizara
ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Fatma Ramadhani alipokuwa akiongea na
wanafunzi wa Shule ya Sekondari Dodoma walipotembelea shule hiyo kwa ajili
kujifunza juu ya mfumo wa ufundishaji mubashara unavyofanya kazi.
Ramadhani
alisema kuwa mfumo wa ufundishaji mubashara unawarahisishia walimu kufundisha
kwa wepesi na wanafunzi kuelewa zaidi kwa sababu wanakuwa wakisikiliza na
kuona. “Hivyo, ni jukumu lenu sasa wanafunzi kuweza kuhakikisha mnaitumia
vizuri teknolojia hii si kwa maisha yenu pekee, bali kwa vizazi vijavyo. Kwasababu
leo ni mwanafunzi lakini ni dada kwenye familia, baadae utabadilika utakuwa
mama kwenye familia yako na pia mtendaji kazi katika jamii yako. Kwa hiyo,
jamii inakusubiri ukaitumikie. Je, utaweza kuitumikia kama haukuelimika? Ili
uelimike lazima ufuatilie haya unayofundishwa kwa makini” alisema Ramadhani.
Wakati
huohuo, Mkurugenzi wa Idara ya Sekondari Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar,
Asya Issa alisema kuwa serikali inawekeza ili wanafunzi waweze kutimiza ndoto
zao katika masomo. “Kwa niaba ya wenzangu kwenye msafara wetu, tunapenda
kuwashukuru uongozi wa Sule ya Sekondari Dodoma kwa mapokezi na kazi nzuri
mnayoifanya. Kwa wanafunzi, wanafunzi mnaona serikali inavyohangaika na walimu
wanavyohangaika kwa ajili yenu ili msome vizuri na kufikia ndoto zenu.
Hakikisheni mnatendea haki juhudi hizi kwa kusoma kwa bidii na kufikia malengo
yanayotarajiwa na serikali na malengo yenu binafsi” alisema Issa.
Mkurugenzi wa Idara ya Sekondari Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Asya Issa akitoa neno |
Shule
ya Sekondari Dodoma ni moja ya vituo vilivyochaguliwa na kufungwa mfumo
unaowezesha ufundishaji mubashara ambao mwalimu anaweza kuwa shuleni hapo akafundisha
wanafunzi wa shule nyingine wakimuona na kuweza kuuliza maswali na kujibiwa.
MWISHO
Comments
Post a Comment