JAMII DODOMA YASHAURIWA KUSAIDIA WATOTO WENYE MAHITAJI MAALUM
Na.
Dennis Gondwe, HOMBOLO BWAWANI
JAMII
imeshauriwa kutenga muda kuwasaidia watoto wenye mahitaji maalum katika Halmashauri
ya Jiji la Dodoma ili waweze kujimudu na kufikia malengo ambayo taifa
linapenda.
Mdau wa elimu katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Mwl. Tatu Mwangu akimpatia zawadi mtoto |
Kauli
hiyo ilitolewa na mdau wa elimu katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Mwl. Tatu
Mwangu alipoungana na Jumuiya ya Shule ya Msingi Feza tawi la Dodoma kutoa
msaada wa viti mwendo nane na vifaa vya elimu kwa watoto wenye mahitaji maalum katika
Shule ya Msingi Hombolo Bwawani.
Mwl.
Mwangu alisema “katika hali ya kawaida sisi kama jamii tunawajibika kuwasaidia
wote wasio na uhitaji na wenye uhitaji maalum kufikia ndoto zao. Leo kupitia
familia ya Shule ya Feza wamepewa vifaa vya kuwasaidia katika kujifunza na
kuweza kutembea kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine kwa wale wenye
changamoto ya viungo. Tuishukuru familia ya Shule ya Feza kwa kutushirikisha
wazazi. Kwa kufanya hivyo kila mwaka tunakusanya kama sadaka kwa ajili ya
watoto wenye uhitaji sehemu mbalimbali. Kwa mwaka huu Hombolo Bwawani tumeipa
kipaumbele na mpokee hiki tulichokileta kwenu. Tuwashukuru viongozi ngazi ya kata,
halmashauri na kitaifa kwa kutambua umuhimu wa elimu kwa watoto wenye mahitaji
maalum. Kwa juhudi wanazoendelea kuzitoa kuhakikisha watoto hawa wanakuwa
salama na wanafikia yale malengo ambayo tunayatarajia”.
Alisema
kuwa watoto hao wana uhitaji wa kusaidiwa. “Kutokana na umuhimu huo tunaona ni
thamani kubwa sana tuwapende kama tunavyojipenda sisi, tuwapende watoto wetu
hawa na tuwasaidie walimu kwa kushirikiana na wazazi. Kuhakikisha mafanikio ya
kitaifa yanafikiwa na mafanikio ya kielimu kwa watoto hawa yanafikiwa” alisema
Mwl. Mwangu kwa hisia.
Kwa
upande wake Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Hombolo Bwawani, Mwl. Pascal Ngoda
aliwakaribisha wageni hao na kuwashukuru kwa zawadi.
Aliwataarifu
kuwa serikali inatambua haki na usawa kwa watoto wenye mahitaji maalum. “Mpaka
sasa tuna watoto wenye mahitaji maalum ya aina tano tofauti. Tuna watoto wenye
ulemavu wa viungo, ambao tunashukuru wageni wetu wametuletea viti mwendo kwa
ajili ya kuwasaidia kutembea kutoka bwenini hadi shuleni. Lakini pia watoto
wenye ulemavu wa ngozi yaani albino, lakini tuna watoto wenye changamoto ya
akili. Tuna watoto wenye uono afifu na watoto wasioona kabisa. Msisite
kututembelea nyie ni sehemu ya faraja kwetu sisi mnapokuja mara kwa mara hata
bila chochote sisi tunawakaribisha na tunawapokea tunatamani na tunajiona sisi
ni sehemu ya jamii” alisema Mwl. Ngoda.
Akishukuru
kwa niaba ya watoto wenye mahitaji maalum, Dickson Frank alisema kuwa Mungu
awabariki wageni hao. “Kwa niaba ya wanafunzi wenzangu napenda niwashukuru
wageni wetu mliokuja kututembelea leo Mungu awabariki na awaongezee pale
mlipopunguza. Kwenu mnaona ni kidogo lakini kwetu tunaona ni kikubwa sana.
Mwenyezi Mungu atembee nanyi awape mkono katika safari yenu. Sisi hatukutarajia
tutaletewa kitu kama hiki ila tunashukuru sana Shule ya Feza. Wengine walikuwa
hawana viti mwendo sasa tumepata kwa ajili ya kuwatembeza wenzetu” alisema kwa
sauti ya shukrani.
MWISHO
Comments
Post a Comment