WAZAZI SHULE YA FEZA DODOMA WAPONGEZWA KUCHANGIA WATOTO WENYE MAHITAJI MAALUM
Na. Dennis Gondwe, HOMBOLO BWAWANI
WAZAZI
wa Shule ya Msingi Feza na jamii wamepongezwa kwa kuchangia watoto wenye mahita
maalum kwa moyo na upendo sababu ni sehemu ya jamii jambo linalowapa faraja
watoto.
Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Shule ya Msingi Feza Dodoma, Mariam Mafuru akiongea na jumuiya ya Shule ya Msingi Hombolo Bwawani |
Kauli
hiyo ilitolewa na Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Shule ya Msingi Feza Dodoma,
Mariam Mafuru alipokuwa akitoa salamu za shule hiyo kwa Jumuiya ya Shule ya Msingi
Hombolo Bwawani alipoongoza ujumbe wa shule hiyo kupeleka zawadi kwa wanafunzi
wenye mahitaji maalum katika Kata ya Hombolo Bwawani.
Mafuru
alisema “napenda kuchukua nafasi hii kuwashukuru wazazi wenzangu tulioweza
kushikiri na kujitoa kwa hali, mali na muda kuweza kuchangia zoezi hili na
hatimae leo mafanikio yameonekana. Hiki kinachoonekana mbele yetu ni nguvu zetu
sote, wazazi tumeshirikiana kwa pamoja tumeweka moyo na upendo kwa ajili ya
kuwasaidia watoto wetu wapendwa. Kama familia ya Shule za Msingi Feza Dodoma
tuna utaratibu wa kujumuika na wenzetu kwa kile kidogo ambacho Mwenyezi Mungu
anakuwa ametubariki. Kwa mwaka huu tulifanya ‘Charity Marathon’ ambayo lengo
kubwa ilikuwa kuelekeza kile kitakachopatikana kwa wale wenzetu wenye uhitaji
maalum”.
Aidha,
aliushukuru uongozi wa Shule ya Msingi Feza kwa kuwafanya wazazi sehemu ya
kuisaidia jamii katika jambo jema. “Tunaomba tuendelee kushirikiana nao
wasituache kwa sababu ni sehemu ya huduma. Tukumbuke kwamba tunao wale watoto wa
kwetu, lakini hiki tulichokifanya ni kikubwa kuliko kile tunachokifanya kwa
wale wa kwetu siku zote. Tutembee nao watoto ni taifa kubwa, watoto ni tegemezi
sana na tunawategemea katika maendeleo ya taifa letu. Tuishi tukiwakumbuka,
nashukuru sana kuwa sehemu ya hii familia” alisisitiza Mafuru.
Akiwasilisha
taarifa fupi ya shule, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Hombolo Bwawani, Mwl.
Pascal Ngoda alisema kuwa hiyo ni shule jumuishi ambayo inahusisha watoto wa
kawaida na watoto wenye mahitaji maalum.
![]() |
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Hombolo Bwawani, Mwl. Pascal Ngoda akitoa maelezo ya shule yake |
“Kutokana
na jitihada za serikali na kutambua haki na usawa kwa watoto wenye mahitaji
maalum mpaka sasa tuna watoto wenye mahitaji ya aina tano tofauti. Tuna watoto
wenye ulemavu wa viungo, ambao tunashukuru wageni wetu wametuletea viti mwendo
kwa ajili ya kuwasaidia kutembea kutoka bwenini hadi shuleni. Lakini pia watoto
wenye ulemavu wa ngozi yaani Albino, lakini tuna watoto wenye changamoto ya
akili. Tuna watoto wenye uono hafifu na tuna watoto wasioona kabisa. Msisite
kututembelea, nyie ni sehemu ya faraja kwetu sisi, mnapokuja mara kwa mara hata
bila chochote sisi tunawakaribisha na tunawapokea, tunatamani na tunajiona sisi
ni sehemu ya jamii” alisema Mwl. Ngoda.
Akitoa
shukrani, Diwani wa Kata ya Hombolo Bwawani, Ased Ndajiro alitoa shukrani kwa
uongozi wa Shule ya Msingi Feza Dodoma kwa kuwapelekea zawadi wanafunzi wenye
mahitaji maalum na kusema kuwa hiyo ni faraja kwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
“Napenda kumshukuru sana Mwenyezi Mungu, Mheshimiwa Rais, Samia Suluhu Hassan,
Mbunge Anthony Mavunde. Sina budi kushukuru Shule ya Msingi Feza kwa kutuletea
msaada wa viti mwendo na vifaa vitakavyowasaidia kwenye mwendo na kwenye masomo
yao, kama mnavyowaona watoto wengine kunyanyuka ni shida. Nisisitize pia kwa
yeyote anayewiwa na ana uwezo na nguvu hawa ni watu wanaohitaji mahitaji ya
faraja, fedha, nguo na afya na mambo mengine ambayo mtu ataguswa nayo” alisema Ndajiro.
Ikumbukwe
kuwa shule hiyo ilianza kama kituo cha watoto wenye ulemavu wa ngozi mwaka 1972.
MWISHO
Comments
Post a Comment