VYOMBO VYA HABARI JIJI LA DODOMA VYAPONGEZWA KUJALI WENYE MAHITAJI MAALUM
Na.
Dennis Gondwe, HOMBOLO BWAWANI
VYOMBO
vya habari katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma vimepongezwa kwa utayari wao
kutangaza mafanikio na changamoto wanazopitia watoto wenye mahitaji maalum
katika Shule ya Msingi Hombolo Bwawani.
Diwani wa Kata ya Hombolo Bwawani, Ased Ndajilo akikabidhi zawadi kwa watoto wenye mahitaji maalum |
Diwani wa Kata ya Hombolo Bwawani, Ased Ndajilo akihamasisha jamii kuchangia watoto wenye mahitaji maalum |
Pongezi
hizo zilitolewa na Diwani wa Kata ya Hombolo Bwawani, Ased Ndajilo alipokuwa
akitoa shukrani kwa Jumuiya ya Shule ya Msingi Feza tawi la Dodoma
walipotembelea Shule ya Msingi Hombolo Bwawani kutoa zawadi ya viti mwendo nane
na vifaa vya elimu kwa watoto wenye mahitaji maalumu wa Shule ya Msingi Hombolo
Bwawani.
Ndajilo
alisema “napenda kumshukuru sana Mwenyezi Mungu, Mheshimiwa Rais, mama yetu
Samia Suluhu Hassan, Mbunge na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde kwa kazi nzuri
wanayofanya katika Kata ya Hombolo Bwawani. Sina budi kushukuru Shule ya Msingi
Feza kwa kutuletea msaada wa viti mwendo nane na vifaa vitakavyowasaidia watoto
kwenye mwendo na kwenye masomo yao, kama mnavyowaona wengine kunyanyuka ni
shida. Hii ni faraja sana kwetu Halmashauri ya Jiji la Dodoma, tunapenda kutoa
pongezi na shukurani kwa Shule ya Msingi Feza”.
Aidha,
alivishukuru vyombo vyote vya habari ambavyo vimekuwa vikitangaza mafanikio na
changamoto za shule hiyo na kuwavuta wanajamii kutoa msaada. “Nisisitize pia
kwa yeyote anayewiwa akiwa na uwezo na nguvu, hawa ni watu wanaohitaji mahitaji
ya faraja, fedha, nguo na afya na mambo mengine ambayo mtu ataguswa nayo. Kwa
hiyo mimi mwenye kata nina wakaribisha wote wenye kuguswa wanaweza kuja na
kuchangia kadri wanavyo weza” alisisitiza Ndajilo.
Kwa
upande wake Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Hombolo Bwawani, Mwl. Pascal Ngoda
aliwakaribisha wageni hao na kuwashukuru kwa zawadi.
Aliwataarifu
kuwa serikali inatambua haki na usawa kwa watoto wenye mahitaji maalum. “Mpaka
sasa tuna watoto wenye mahitaji maalum ya aina tano tofauti. Tuna watoto wenye
ulemavu wa viungo, ambao tunashukuru wageni wetu wametuletea viti mwendo kwa
ajili ya kuwasaidia kutembea kutoka bwenini hadi shuleni. Lakini pia watoto
wenye ulemavu wa ngozi yaani albino, lakini tuna watoto wenye changamoto ya
akili. Tuna watoto wenye uono afifu na watoto wasioona kabisa. Msisite
kututembelea nyie ni sehemu ya faraja kwetu sisi mnapokuja mara kwa mara hata
bila chochote sisi tunawakaribisha na tunawapokea tunatamani na tunajiona sisi
ni sehemu ya jamii” alisema Mwl. Ngoda.
Akishukuru
kwa niaba ya watoto wenye mahitaji maalum, Dickson Frank alisema kuwa Mungu
awabariki wageni hao. “Kwa niaba ya wanafunzi wenzangu napenda niwashukuru
wageni wetu mliokuja kututembelea leo Mungu awabariki na awaongezee pale
mlipopunguza. Kwenu mnaona ni kidogo lakini kwetu tunaona ni kikubwa sana.
Mwenyezi Mungu atembee nanyi awape mkono katika safari yenu. Sisi hatukutarajia
tutaletewa kitu kama hiki ila tunashukuru sana Shule ya Feza. Wengine walikuwa
hawana viti mwendo sasa tumepata kwa ajili ya kuwatembeza wenzetu” alisema kwa
sauti ya shukrani.
Jumuiya ya Shule ya Msingi Feza tawi la Dodoma
ilifanya Charity Marathon na kukusanya fedha na kuchangia viti mwendo nane na
vifaa vingine vya elimu kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalum wa Shule
ya Msingi Hombolo Bwawani jijini Dodoma.
MWISHO
Comments
Post a Comment