JIJI LA DODOMA LAMSHUKURU DKT. SAMIA KUJALI WATOTO WENYE MAHITAJI
Na.
Dennis Gondwe, HOMBOLO BWAWANI
HALMASHAURI
ya Jiji la Dodoma imemshukuru Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwajali
watoto wenye mahitaji maalum.
Shukrani
hizo zilitolewa na Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Mwl.
Issa Kambi katika hafla ya kupokea viti mwendo na vifaa vya shule kwa watoto
wenye mahitaji maalum katika Shule ya Msingi Hombolo Bwawani iliyopo jijini
Dodoma.
Mwl. Kambi alisema “tunamshukuru Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa
anayoifanya kwa watoto hawa wenye mahitaji maalum katika Halmashauri ya Jiji la
Dodoma. Mfano, katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma Mheshimiwa Rais kupitia Ofisi
ya Rais, Tamisemi anatuletea shilingi 26,000,000 kila mwezi kwa ajili ya
chakula cha watoto hawa. Tunapopata wadau kuja kuunga mkono juhudi za Mheshimiwa
Rais tunafurahi sana. Kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma,
John Kayombo aliyeniagiza niwashukuru kwa kutusaidia. Na yeye kwa mwaka huu
ametenga shilingi 20,000,000 kwa ajili ya vifaa vya watoto hawa wenye mahitaji
maalum katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma”.
Akiongelea
msaada wa vifaa vilivyotolewa na Shule ya Msingi Feza, alisema kuwa halmashauri
imekuwa ikipokea vifaa kwa ajili ya watoto wenye mahitaji maalum kila mwaka.
“Na msimu huu wamefanya jambo kubwa zaidi kutuletea viti mwendo nane kwa watoto
wetu hawa ambao baadhi viti vyao vilikuwa vimechakaa na wengine walikuwa hawana
kabisa. Hili ni jambo zuri na kuunga mkono juhudi za Mheshimiwa Rais, Dkt.
Samia Suluhu Hassan” alisema Mwl. Kambi.
Mwl. Kambi alisema kuwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma ina vituo 10 vyenye watoto watoto wenye mahitaji maalum. “Nimshukuru pia Diwani wa Kata ya Hombolo Bwawani ambae tupo nae hapa kwa kazi nzuri anayoifanya kuendelea kuwalea hawa watoto na kusaidia kwenye ujenzi wa miundombinu. Tunakushukuru sana Mheshimiwa Diwani” alisema Mwl. Kambi.
Kwa
upande wake Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Hombolo Bwawani, Mwl. Pascal Ngoda
aliwakaribisha wageni hao na kuwashukuru kwa zawadi.
Aliwataarifu
kuwa serikali inatambua haki na usawa kwa watoto wenye mahitaji maalum. “Mpaka
sasa tuna watoto wenye mahitaji maalum ya aina tano tofauti. Tuna watoto wenye
ulemavu wa viungo, ambao tunashukuru wageni wetu wametuletea viti mwendo kwa
ajili ya kuwasaidia kutembea kutoka bwenini hadi shuleni. Lakini pia watoto
wenye ulemavu wa ngozi yaani albino, lakini tuna watoto wenye changamoto ya
akili. Tuna watoto wenye uono afifu na watoto wasioona kabisa. Msisite
kututembelea nyie ni sehemu ya faraja kwetu sisi mnapokuja mara kwa mara hata
bila chochote sisi tunawakaribisha na tunawapokea tunatamani na tunajiona sisi
ni sehemu ya jamii” alisema Mwl. Ngoda.
Akishukuru
kwa niaba ya watoto wenye mahitaji maalum, Dickson Frank alisema kuwa Mungu
awabariki wageni hao. “Kwa niaba ya wanafunzi wenzangu napenda niwashukuru
wageni wetu mliokuja kututembelea leo Mungu awabariki na awaongezee pale
mlipopunguza. Kwenu mnaona ni kidogo lakini kwetu tunaona ni kikubwa sana.
Mwenyezi Mungu atembee nanyi awape mkono katika safari yenu. Sisi hatukutarajia
tutaletewa kitu kama hiki ila tunashukuru sana Shule ya Feza. Wengine walikuwa
hawana viti mwendo sasa tumepata kwa ajili ya kuwatembeza wenzetu” alisema kwa
sauti ya shukrani.
Ikumbukwe kuwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma ina watoto wenye mahitaji maalum 1,050 na Shule ya Msingi Hombolo Bwawani ikiwa na watoto 44 wenye mahitaji maalum.
MWISHO
Comments
Post a Comment