JIJI LA DODOMA LAZINDUA ZOEZI LA UBAINISHAJI WATOTO WENYE MAHITAJI MAALUM
Na. Dennis Gondwe, HOMBOLO BWAWANI
Halmashauri ya Jiji la Dodoma
imezindua zoezi la ubainishaji watoto wenye mahitaji maalum katika jamii ili
waweze kupata haki yao ya elimu na matunzo kwa mujibu wa sheria.
Kauli hiyo ilitolewa na Mwakilishi
wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Issa Kambi alipokuwa akizindua
zoezi la ubainishaji watoto wenye mahitaji maalum katika jamii uzinduzi
uliofanyika katika Shule ya Msingi Hombolo Bwawani iliyopo Kata ya hombolo
Bwawani jijini Dodoma.
Kambi ambae ni Afisa Elimu
Maalum katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma alisema “kwa niaba ya Mkurugenzi wa
Halmashauri ya Jiji la Dodoma ambae alipenda sana kuwa nasi hapa leo napenda
kuzindua rasmi zoezi la ubainishaji watoto wenye mahitaji maalum kwa maana ya kwenda
kuwatafuta mtaani na kuwaleta kwenye vituo vyetu kama hiki na vitengo vingine. Zoezi
litafanyika katika mitaa nane ya Itega, Salama, Lugala, Mnyakongo, Mtube, Nala,
Chigongwe na Mbalawala”.
Alisema kuwa lengo la
zoezi hilo ni kuwabaini watoto hao mahali walipo na kuwasogeza kwenye huduma na
kuwapatia afua stahiki ikiwa ni pamoja na elimu na matunzo. “Tunafahamu kwamba
baadhi ya familia zinaamini watoto hawa hawawezi kufanya mambo, lakini
tunapokwenda kufanya ubainishaji tunawatia moyo na kuwashawishi kuwaleta watoto
hawa shule. Kuanzia ngazi za familia tunapeleka elimu na baadae tunawaleta
kwenye vituo kama hivi na kama mlivyoona watoto hawa wanafuraha” alisema Kambi.
Akiongelea umuhimu wa
zoezi hilo, Mkazi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma Juliana Linus alisema kuwa
zoezi hilo ni muhimu kwa sababu linakwenda kuwapatia haki ya msingi watoto
wenye mahitaji maalum katika Jiji la Dodoma. “Ni kweli wapo baadhi ya wazazi
ambao wamekuwa na tabia ya kuwaficha watoto wao wenye ulemavu jambo
linalowanyika haki watoto hao kupata elimu, afya na malezi bora” alisema Linus.
Zoezi la uzinduzi wa
ubainishaji watoto wenye mahitaji maalumu katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma lilihudhuriwa
na Jumuiya ya Shule ya Msingi Hombolo Bwawani ambayo ni shule jumuishi, Diwani
wa Kata ya Hombolo Bwawani, maafisa waandamizi kutoka Halmashauri ya Jiji la Dodoma
na wawakilishi wa Jumuiya ya Shule ya Msingi Feza tawi la Dodoma na wawakilishi
wa serikali ya mtaa.
MWISHO
Comments
Post a Comment