Ujenzi Shule za Sekondari za ziada Suluhu Changamoto ya Umbali
Na. Faraja Mbise, DODOMA
Kata 41 za Halmashauri ya Jiji la Dodoma
zinatarajiwa kunufaika na ujenzi wa shule za sekondari za ziada kwa ajili ya
kuhakikisha mtoto anapata elimu katika mazingira mazuri na kutatua changamoto
ya umbali wa kupata huduma ya elimu.
Hayo yalisemwa na Mbunge wa Dodoma
Mjini, Anthony Mavunde, alipokuwa akitoa hotuba kwa madiwani, wakuu wa divisheni
na vitengo, walimu, watendaji wa kata na wanafunzi waliohudhuria katika hafla
ya Ugawaji Kompyuta na Printa kwa Shule za Sekondari na maafisa watendaji wa
kata jijini Dodoma.
Mbunge wa Jimbo la Dodoma, Anthony
Mavunde alisema “moja kati ya mipango yangu mikubwa nayoendelea nayo ni
kuendelea kuhakikisha kata zote za Dodoma zina sekondari, tukimaliza hayo
tuongeze sekondari za ziada hasa zile ambazo watoto wanatembea umbali mrefu.
Mheshimiwa mkuu wa wilaya ukienda pembezoni mwa Jiji la Dodoma, kuna maeneo
ambayo watoto walikuwa wanatembea mpaka kilomita 16 kufuata shule. Ukienda Kata
ya Chahwa eneo la Mahoma Makulu watoto walikuwa wanatembea umbali mrefu kwenda
Ipala Sekondari”.
Kwa upande wake Mkuu wa Shule ya Sekondari
Anthony Mavunde, Mwl. Emmanuel Magumba, alimshukuru Mbunge wa Dodoma Mjini kwa
ugawaji wa Printa na Kompyuta kwasababu itaenda kutatua changamoto waliyokuwa
wanaipata awali katika uandaaji wa mitihani.
“Zoezi hili la ugawaji Kompyuta na
Printa nimelipokea kwa mikono miwili na linakwenda kuongeza hali ya utoaji wa
mitihani shuleni kwetu kwasababu tulikuwa hatuna vifaa kwa ajili ya kuandalia
mitihani na uchapishaji. Hili linakwenda kusaidia wanafunzi wetu kupata elimu
bora hasa katika upataji wa mitihani, utoaji wa notisi pamoja na vifaa ambavyo
vimewekwa humu kwa ajili ya kusaidia watoto” alisema Mwl. Magumba.
Nae, mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Umonga, Angelina Masikini alimshukuru Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini kwa ujio wake na kugawa kompyuta na printa kwa shule zilizopo jijini Dodoma. “Tunamshukuru Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini, Anthony Mavunde kwa kufanya Hafla hii ya Ugawaji wa Kompyuta na Printa kwa Shule za Sekondari jijini Dodoma, tunaamini vifaa hivi vitaenda kuongeza ujuzi wetu darasani na kutupa uwezo mkubwa wa kuendena na mabadiliko ya kiteknolojia yanayoendelea hivi sasa” alishukuru Masikini.
MWISHO
Comments
Post a Comment