Mkutano Mkuu wa 39 wa ALAT wafanyika Dodoma
Na. Aisha Ibrahim, DODOMA
Mkutano
mkuu wa 39 wa Mwaka wa Mamlaka ya Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT)
umefanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete Convention Center jijini
Dodoma, uliofunguliwa na mgeni rasmi ambaye ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa lengo la kujadili na kufanya tathmini
ya mipango ya ALAT na mambo mbalimbali yanayoendelea katika serikali za mitaa.
Akitoa taarifa wakati wa mkutano huo, Mwenyekiti wa ALAT Taifa, Murshid Ngeze, alisema kuwa katika mkutano wa mwaka huo wamejitahidi kualika viongozi mbalimbali wakiwemo wenyeviti wa mitaa ili kupata maarifa mbalimbali yanayohusiana na uendeshaji wa serikali za mitaa. Hivyo, kwenda kuwa viongozi bora katika mitaa yao. “Mkutano huu tunafanya kila mwaka, lakini mwaka huu tumeenda mbali zaidi kwa kuwaalika wenyeviti wa serikali za mitaa ili watakapofika hapa waweze kupata ujumbe wa moja kwa moja na kujifunza namna ya uendeshaji na utekelezaji wa shughuli zote zinazohusiana na serikali za mitaa” alisema Ngeze.
Katika
hatua nyingine, aliishukuru Benki ya NMB kwa kuwa mdau mkubwa wa ALAT na
kujitoa katika kuhakikisha shughuli za serikali za mitaa zinazidi kusonga mbele
na kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia
Suluhu Hassan za kutekeleza miradi mbalimbali nchini. “Tunaishukuru sana Benki
ya NMB kwa kuwa mdau wetu mkubwa na kwa mwaka huu ametuunga sana mkono na
ifikapo tarehe 13 Machi, 2025 wajumbe wote wa mkutano huu tutakuwa tunasafiri
na SGR kutoka Dodoma kwenda Dar es Salaam kwa ufadhiri wa NMB” alishukuru.
Aidha,
aliongeza kuwa ALAT imeimalika na kuwa bora kuliko miaka iliyopita kwasababu taarifa
za ukaguzi zinawasilishwa mbele ya hadhara na kutolewa ufafanuzi
unaojitosheleza. “Mheshimiwa Rais, kwa sasa ALAT imeimarika, mikutano iliyopita
taarifa za ukaguzi zilikuwa haziwasilishwi, lakini hivi sasa taarifa hizi
zinakuwa wazi na kuwasilishwa vizuri sana” aliongeza Ngeze.
Sambamba
na hayo, alifafanua kuwa wamejitahidi kufuata maelekezo ya Rais. Dkt. Samia
Suluhu Hassan ya kuimarisha ushirikiano mzuri kati ya viongozi wa ALAT na
taasisi mbalimbali duniani kote. “Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan
kwanza ulisema tuimarishe ushirikiano wa ALAT na taasisi nyingine ikiwemo;
Umoja wa Serikali za Mitaa Afrika Mashariki na duniani kote. Hivyo,
nikuthibitishie kwamba kauli yako tumeitekeleza kama unavyoona hapa wapo
viongozi wa ALAT kutoka Zanzibar na Afrika Mashariki” alifafanua.
Pia
alieleza kuwa wamejitahidi kuimarisha ukusanyaji wa mapato kwenye Mamlaka ya
Serikali za Mitaa. “Hapo nyuma tulikusanya kiasi cha shilingi bilioni 848 kwa
mwaka wa fedha 2024/2025 ikiwa ni sawa na asilimia 60 ndani ya halmashauri zetu
nchini, na hii yote ni kutekeleza maelekezo ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan” alieleza
Ngeze.
Alimaliza
kwa kusema kuwa “tunafanya kazi kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo ya
ALAT, na hivi sasa tumeenda mbali zaidi kupitia mkutano huu tunakwenda kuhuisha
sheria ya uanzishaji wa ALAT na iendelee kuimarika chini ya ushirikiano mkubwa
kuhakikisha maendeleo ya wananchi yanatekelezeka” alisema Ngeze.
MWISHO
Comments
Post a Comment