Dkt. Sagamiko asema, ugawaji jimbo hauna athari kwa huduma zinazotolewa na Jiji la Dodoma
Na, Nancy Kivuyo, DODOMA
Mkurugenzi
wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dkt. Frederick Sagamiko alitoa hofu Baraza la
Madiwani kuwa kukidhi vigezo vya ugawaji wa Jimbo la Dodoma Mjini hauna athari
katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo katika kuwahudumia wananchi.
Aliyasema hayo wakati akijibu hoja za madiwani waliohudhuria katika Mkutano maalum wa Baraza la Madiwani kwa ajili ya kupokea taarifa ya mapendekezo ya mgawanyo wa Jimbo la Dodoma Mjini uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa halmashauri.
“Mgawanyo
wa jimbo kwa upande wa tarafa hauna kikwazo chochote, kama ni kata ni kikwazo
kwasababu kata moja haiwezi kuwa katika majimbo mawili. Leo tutaangalia zaidi
kwenye kata” alisema Dkt. Sagamiko.
Aliongeza
kuwa, athari za mgawanyo wa jimbo kimapato unalenga mgawanyo wa majimbo na sio
shughuli za kiutendaji. “Niwatoe wasiwasi, utoaji wa huduma kwa wananchi
utaendelea kama ilivyokua awali na Halmashauri ya Jiji la Dodoma. Baraza
litakua moja bila kujali jimbo analotoka diwani. Mipango itapangwa kulingana na
Halmashauri ya Jiji la Dodoma” alimalizia Dkt. Sagamiko.
Nae,
Diwani wa Kata ya Ihumwa, Edward Magawa, aliishukuru serikali kwa kuleta
mapendekezo ya mgawanyo wa Jimbo la Dodoma Mjini kwakuwa jiografia yake imekua
kubwa na namna ya kuhudumia kata 41 kwa pamoja ni changamoto. “Binafsi
niipongeze serikali kwa namna wameona ni vema kugawanya jimbo ili kupata
urahisi wa kuhudumia wananchi. Nimpongeze pia Mheshimiwa mbunge kwa kazi nzuri,
amejitahidi kuhudumia kata 41 kwa namna alivyoweza lakini sasa itakua rahisi
mbunge kuwafikia wananchi na kutatua changamoto kwa urahisi” alisema Magawa.
Kwa upande mwingine, Diwani wa Viti Maalum, Wendo Kutusha alisema “taarifa hii nimeipokea kwa furaha kubwa sana kwasababu kata 41 alizokua anashughulika nazo mbunge wetu Mavunde ni nyingi mno. Kuna majimbo mengine yana kata chache sana. Kwahiyo, ujio wa mgawanyo huu utasaidia mbunge kuzifikia kata zote. Naishukuru sana Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi kwa kuliona jimbo hili linafaa kuwa na wawakilishi wawili watakaoendeleza maendeleo ya Jiji la Dodoma. Matarajio yangu ni kwamba tunatarajia kuwa shughuli za maendeleo ziwe nyingi na maendeleo yakaonekane katika jamii zetu” alimalizia Kutusha.
Mapendekezo
ya kugawanya Jimbo la Dodoma Mjini lenye jumla ya wapiga kura 795,000 na kuwa
majimbo mawili, Jimbo la Dodoma Mjini lenye jumla ya watu 412,000 na kata 21 na
Jimbo la Mtumba lenye jumla ya watu 383,000 na kata 20 kwa lengo la kusigeza
huduma kwa wananchi ambao ndio msingi wa demokrasia ya uwakilishi ndani ya Wilaya
ya Dodoma yamepokelewa na kupitishwa kwa kauli moja.
MWISHO
Comments
Post a Comment