Kilimo cha Zabibu ni ajira kwa vijana kujikwamua kiuchumi
Na. Nancy Kivuyo, MATUMBULU
Vijana wa Kata ya Matumbulu
wameendelea kunufaika na fursa za mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri
ya Jiji la Dodoma kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu na
kuweza kujikwamua kiuchumi.
Kauli hiyo ilitolewa na Mwenyekiti wa Kikundi cha Kaunda kinachojishughulisha na kilimo cha zabibu, Isack Benjamin alipokuwa akiongea na waandishi wa habari waliofanya media tour kufuatilia wanufaika wa mikopo hiyo katika kata ya matumbulu.
Benjamin alisema kuwa mikopo ya
asilimia nne inayotolewa na halmashauri
imekua mkombozi kwa vijana wanaopenda kujishughulisha na kuingiza kipato ili
kuboresha maisha yao. “Kikundi chetu kilipata mkopo wa shilingi milioni 20,
ambapo tupo vijana watano. Tuliwekeza kwenye kilimo cha zabibu kwasababu tuna
maeneo makubwa huku na kilimo cha zabibu kinakubali sana. Kiukweli, faida
tuliiona, tunasomesha watoto, tunapata mahitaji muhimu na kubwa zaidi tumeweza
kuongeza tena ekari tano ambazo kama mnavyoona tunalima tena zabibu” alisema
Benjamin.
Nae Afisa Kilimo Kata ya Matumbulu,
Aneth Mnana alisema kuwa kata hiyo ina
ardhi nzuri kwa ajili ya kilimo. “Kata ina maji ya kumwagilia mboga mboga na
mazao mengine ya muda mfupi. Hawa wakulima tunawapa elimu ya kutosha ili
kufanya kilimo chenye tija. Ndio maana mnaona kwasasa wanatoa mazao mazuri
sana. Nashauri wataalam wenzangu kuendelea kuwahudumia wananchi kwa weledi ili
kilimo kiwe na tija kwa jamii zote kwa siku za usoni” alisema Mnana.
Kwa upande wake mkulima Mussa Mlilima
aliishukuru serikali kwa elimu ya kilimo kutoka kwa wataalam ambao wameletwa
katika Kata ya Matumbulu na kuahidi kuendelea kufanya kilimo chenye tija ili
kupata mazao bora. “Namshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuongeza watumishi wa kila kada mpaka
kwenye kata zetu. Namshukuru pia Mbunge wetu, Anthony Mavunde na Diwani,
Emmanuel Chibago kwa jitihada zao katika kuhakikisha kata yetu inakua sehemu ya
kilimo bora kwa zabibu na mazao mengine” alisema Mlilima.
MWISHO
Comments
Post a Comment