Kikundi cha Kilasara chanufaika mkopo wa halmashauri
Na. Nancy Kivuyo, MATUMBULU
MIKOPO
isiyo na riba ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa
makundi ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu imekuwa chachu ya kusukuma maendeleo
katika sekta za kilimo, ufugaji na ujasiriamali.
Akizungumza
na waandishi wa habari waliotembelea kikundi hicho kufuatilia manufaa ya mikopo
hiyo kwa jamii, Mwenyekiti wa Kikundi cha Kilasara, Judika Urio alisema kuwa
wanawake hao wamenufaika na mkopo huo usio na riba. “Kikundi chetu tupo watano,
tulipata takribani shilingi milioni 20 ambazo tuliwekeza katika ufugaji wa
kuku, bata mzinga, bata bukini na sungura. Baada ya mafanikio ya ufugaji huo,
tulipata faida ambayo ilituwezesha kuanzisha mradi mwingine wa uzalishaji wa samaki
kama mnavyoona kwenye mabwawa haya, tumeweka mbegu ya samaki wapatao elfu 10
ambao tunategemea baada ya mwaka ndio tuvune” alisema Urio.
Alimshukuru
Rais, kwa kuyajali makundi ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, na kusema
kuwa amewainua na kuwapa kipaumbele. “Namshukuru pia mbunge wetu, Anthony
Mavunde na Diwani, Emmanuel Chibago, tunaamini wana mchango mkubwa katika
kuishauri serikali kuangalia makundi haya katika jamii ili yawezeshwe
kujikwamua kiuchumi” alimalizia Urio.
Nae,
Afisa Maendeleo ya Jamii Kata ya Matumbulu, Merina Gombo, alisema kuwa
wanasaidia makundi ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kupata elimu
sahihi juu ya mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri na kuwasimamia.
“Lengo letu ni kuhakikisha makundi haya yanapata mikopo ya asilimia 10 ili
kujikwamua kiuchumi. Yapo makundi nane yaliyopata mikopo hiyo ikiwemo kikundi
hiki cha Kilasara ambao ni mfano wa kuigwa na akina mama wengine wanaotaka kuja
kukopa na kujiingiza katika shughuli za maendeleo” alisema Gombo.
Kwa
upande mwingine, mnufaika wa ajira kupitia Kikundi cha Kilasara, Furaha Anthony
alisema kuwa anakishukuru kikundi hicho kwa kumpatia ajira. “Ninafuga hawa
samaki katika haya mabwawa tangu mradi huu umeanzishwa. Hawa samaki wanakuwa
kwa muda wa miezi nane hadi mwaka ndio tunawavuna. Kwahiyo, ni mradi mzuri
unatunufaisha sisi wakazi wa Mtaa wa Nyerere” alisema Anthony.
Kata ya Matumbulu ina jumla ya wakazi takribani 11,169, wakijishughulisha na kilimo cha zabibu, ufugaji wa ng’ombe na kilimo cha kisasa cha mbogamboga na matunda.
MWISHO
Comments
Post a Comment