Baraza la Madiwani Jiji la Dodoma lapitisha rasimu ya Sheria ndogo tano
Na. Dennis Gondwe, DODOMA
NAIBU
Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Fadhili Chibago amesema kuwa mchakato wa
kuandaa Sheria ndogo za halmashauri yake ilizingatia miongozo inayoelekeza
uandaaji wa sheria hizo kwa maslahi ya wananchi wa Dodoma.
Naibu Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Fadhili Chibago, akifafanua jambo |
Alitoa kauli hiyo katika Mkutano Maalum wa Baraza la Madiwani kwa ajili ya kupitia rasimu za Sheria ndogo za Halmashauri ya Jiji la Dodoma uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa halmashauri.
Naibu
Meya Chibago alisema kuwa baraza lake limejiridhisha kuwa kila hatua imepitiwa
vizuri ya mchakato wa kuandaa Sheria ndogo za halmashauri. Mchakato ulikuwa
shirikishi na ulianzia hatua za mwanzo kwa mujibu wa miongozo. Kamati za
Maendeleo za Kata hadi vikao vya juu vya halmashauri. “Tumejadiliana kwa kina
na kuheshimu maoni ya kila mtu. Nawahakikishia kuwa yale tuliyojadili leo,
vielelezo vyote vipo kwa mujibu wa miongozo kutokana na umakini wa baraza hili”
alisema Chibago.
Awali
akiwasilisha Rasimu ya Sheria ndogo za Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa niaba
ya Mkurugenzi wa Jiji, Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Sheria, Wakili Cosmas
Nsemwa alisema kuwa serikali za mitaa zimepewa mamlaka ya kutunga Sheria ndogo
chini ya kifungu cha 88 cha Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Miji) Sura
ya 288. “Utaratibu wa kutunga Sheria ndogo kwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma
umeainishwa kwenye kanuni ya 75 ya kanuni za kudumu za Halmashauri ya Jiji la
Dodoma, Tangazo la Serikali Na. 478 la tarehe 1 Julai, 2022” alisema Wakili
Nsemwa.
Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Sheria, Wakili Cosmas Nsemwa aliwasilisha rasimu ya Sheria ndogo |
Aidha,
alisema kuwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma inakusudia kutunga Sheria ndogo tano
kwa ajili ya udhibiti wa shughuli mbalimbali pamoja na kuanzisha vyanzo vipya vya
mapato. “Rasimu zote za Sheria ndogo zimeandaliwa kwa kuzingatia mambo
yafuatayo;- Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa, Sura 290 Kifungu 16 (1) Sheria
ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Miji) Sura ya 288 Kifungu cha 88,89 na 90.
Mwongozo wa Uandishi wa Sheria ndogo wa Mwaka 2022 uliotolewa na Mwandishi Mkuu
wa Sheria, Kanuni ya 75 ya Kanuni za Kudumu za Halmashauri ya Jiji la Dodoma Tangazo
la Serikali Na. 478 la tarehe 1 Julai, 2022, mapendekezo ya idara tumizi, maoni
ya Kamati ya Maendeleo ya Kata (WDC), kata zote na maoni ya wadau mbalimbali”
alisema Wakili Nsemwa.
Kwa
upande wake Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri aliipongeza halmashauri
kwa kuandaa rasimu ya Sheria ndogo vizuri. “Moja ya mambo ya msingi kuacha
alama ni kutungwa kwa Sheria ndogo ili mapato ya serikali yapatikane. Baraza
lazima kujihoji mara mbili kwa nini kuanzisha Sheria ndogo hizi” alisema
Shekimweri.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri |
Aidha, alielezea sababu za kushindwa kutekelezeka kwa Sheria ndogo kuwa ni uzembe wa kuzisimamia Sheria hizo. “Kama kusipokuwepo na uwezeshwaji vitendea kazi na rasilimali fedha, mfumo wa ufuatiliaji, elimu na uhamasishaji wananchi kuzingatia Sheria ndogo, hizi sheria hazitatekelezeka na itakuwa kazi bure kuandaa mipango isiyotekelezeka” alisema.
Sheria
ndogo tano zilizopitishwa na Mkutano wa Baraza la madiwani ni Sheria Ndogo ya
(Ada na Ushuru) ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma ya Mwaka 2024; Sheria Ndogo ya
(Ushuru wa Madini ya Ujenzi) ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma ya Mwaka 2024;
Sheria Ndogo ya (Ushuru wa Usimamizi na Uendeshaji wa Masoko), Minada na Magulio)
ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma ya Mwaka 2024; Sheria Ndogo ya (Maegesho na
Udhibiti wa Vyombo vya Usafiri) ya Halmashauri ya Jiji ya Mwaka 2024; Sheria
Ndogo ya (Ada na vibali vya shughuli za kiutamaduni) ya Halmashauri ya Jiji la
Dodoma ya Mwaka 2024
MWISHO
Comments
Post a Comment