Waziri Mchengerwa apongeza usimamizi wa miradi jijini Dodoma
Na. Aisha Ibrahim, DODOMA
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za
Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa (Mb), aliwapongeza
watumishi wa umma kwa kusimamia miradi mbalimbali jijini Dodoma ikiwa ni kuunga
mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu
Hassan.
Aliyasema hayo katika Hafla ya utiaji
saini mkataba wa ujenzi wa Soko Kuu la Majengo pamoja ujenzi wa kituo cha
daladala eneo la Mshikamano, Kizota na Nzuguni, iliyofanyika kiwanja cha
Chinangali Park, Jijini Dodoma.
Akizungumzia kuhusu utekelezaji wa miradi
mbalimbali Mohamed Mchengerwa, alitaka wakandarasi wote ambao hawajatekeleza
majukumu yao katika miradi mbalimbali ikiwemo mradi wa ujenzi wa barabara,
kutopewa fursa ya kufanya kazi
yoyote ikiwa ni onyo kwa wale wote
wanaofanya kazi kwa uzembe na kushindwa kutekeleza majukumu yao kwa wakati.
"Maelekezo yangu kwa mtendaji mkuu na
katibu mkuu wa TARURA, Mkandarasi huyu asiruhusiwe kufanya kazi yoyote chini ya
TARURA kuanzia sasa mpaka akamilishe mradi huu tunaoukusudia, pamoja na wengine
ambao hawajakamilisha miradi hii ambayo ilipaswa ikamilike mwezi Februari,
wasiruhusiwe kufanya kazi yoyote hata ya shilingi 500" alisema Mchengerwa.
Sambamba na hayo, alisisitiza kuwepo kwa
utaratibu mzuri wa kuingia na kutoka katika eneo la Stesheni ya reli Jijini
Dodoma ili wananchi na hata wageni
kutoka nje ya Dodoma wajivunie uwepo wa Stesheni hiyo.
"Nawataka wakurugenzi wote wa majiji
hasa Mkurungezi wa Jiji hili la Dodoma ambapo ni makao makuu ya nchi, mkuu wa
Mkoa, Mkuu wa wilaya nendeni pale eneo la Stesheni ya reli na muweke utaratibu
mzuri wa kuingia eneo hilo ili watanzania wanaokwenda na kurudi Jiji la Dodoma
waweze kulifurahia jiji hili" alisema Mchengerwa.
Kwa upande wake Waziri wa madini, Anthony Mavunde
(Mb) alisema kuwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma ndiyo inayoongoza kwa mtandao
mkubwa wa barabara zenye kiwango cha lami ambazo zina jumla ya urefu wa
Kilomita 249.12 nchini Tanzania.
"Katika Halmashauri zote nchi nzima,
Halmashauri ya Jiji la Dodoma ndiyo inaongoza kwa mtandao mrefu wa barabara za
kiwango cha lami, sisi tuna Kilomita 249.12 ikifuatiwa na Halmashauri ya wilaya
ya Kinondoni, wana urefu wa barabara wenye Kilomita 223" alisema Mavunde.
Aidha, aliendelea kwa kusema kuwa kumekuwa
na kero mbalimbali katika vivuko vya maji katika maeneo ya Chaduru, Maili Mbili
na Ntyuka ikiwemo wanafunzi kukwama na kushindwa kupita katika vivuko hivyo
wakati wa mvua jambo linalopelekea kutofika
shuleni kwa wakati.
"Vivuko hivi imekuwa ni kilio
kikubwa, mvua inaponyesha watoto wanaotoka upande wa pili wamekuwa wakishindwa
kuvuka lile Korongo na wamekuwa wakishindwa kwenda shule" alisema Mavunde.
Nae, Mtendaji mkuu, Wakala wa Barabara
Mijini na Vijijini (TARURA), Mhandisi Victor Seif, alisema lengo kuu la mradi
wa "TACTIC" ni kuboresha usimamizi wa ukuaji wa miji pamoja na
kuziwezesha Halmashauri za miji na majiji kutoa huduma bora kwa wananchi
ikiwemo ujenzi wa miundombinu.
Alifafanua kuwa, kazi za ujenzi
zinazofanyika katika mkataba wa "Package 1" ni Barabara ya Mbuyuni
SP2 (Kilomita 1.69), Barabara ya Mauma-Makutano (Mita 760), Barabara ya
Mbuyuni-Mwangaza (Kilomita 2.56), Barabara ya Ntyuka-Mkalama-Mapinduzi
(Kilomita 5.2), Mtaro wa maji ya mvua Ilazo (Kilomita 2.1) na Uboreshaji wa
mabwawa ya kuhifadhia maji ya mvua (3)
na mitaro ya kutiririsha maji (Kilomita 2.81).
Lakini, aliongeza kuwa kazi za ujenzi
zinazotarajiwa kufanyika katika Mkataba wa "Package 2 ni Uboreshaji wa
Soko Kuu la Majengo pamoja na kituo cha daladala eneo la Mshikamano, Uboreshaji
wa Stendi ya mabasi madogo eneo la Kizota, Uboreshaji eneo la mabasi madogo
eneo la Nzuguni na Ujenzi wa Vivuko maji katika maeneo ya Chaduru, Mailimbili
na Ntyuka.
Katika eneo la mabasi madogo (daladala)
kutakuwa na maeneo matatu yaliyopangiwa kwaajili ya daladala kuruhusu urahisi
wa kuingia na kutoka yenye makinga mvua au jua, taa za kutumia umeme jua, choo
cha kulipia na eneo litakaloweza kupangwa wafanyabiashara.
MWISHO
Comments
Post a Comment