Wakandarasi Wasiomaliza Miradi Mashakani
Na. Faraja Mbise, DODOMA
TARURA
imeagizwa kuwasimamisha wakandarasi wasiokamilisha miradi kwa wakati na
wasipewe tena miradi hiyo kwasababu wanakwamisha juhudi za Rais, Dkt. Samia
Suluhu Hassan, katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati na ya
kimaendeleo nchini.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mohamed Mchengerwa (Mb)
Hayo
yalisemwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
(TAMISEMI) Mohamed Mchengerwa (Mb) alipokuwa akizungumza na wataalam kutoka
taasisi mbalimbali za kiserikali pamoja na wananchi wa Jiji la Dodoma katika
Hafla ya utiaji saini mkataba wa uboreshaji Soko Kuu la Majengo pamoja na
ujenzi wa Kituo cha Daladala eneo la Mshikamano, Kizota na Nzuguni, uliofanyika
tarehe 06 Februari, 2025 katika viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma.
“Maelekezo
yangu kwa TARURA, mkandarasi huyu asiruhusiwe kufanya kazi yoyote chini ya
TARURA kuanzia sasa mpaka akamilishe mradi huu tunaoukusudia. Nendeni makafanye
tathmini, mniletee taarifa maramoja” alielekeza Mchengerwa.
Kauli
hiyo, ilifuatiwa mara baada ya Waziri wa Madini, Anthony Mavunde (Mb) kutoa
lalamiko la kutokukamilika kwa mradi uliokabidhiwa tarehe 23 Septemba, 2023,
Mkandarasi huyo alipatiwa kiasi cha fedha Milioni 24 kwa awamu ya kwanza na
kutakiwa kukamilisha mradi huo kwa wakati.
Sambamba
na hilo alitoa agizo kwa wakandarasi wote nchini, ambao hawakamilishi miradi
yao kwa wakati uliowekwa katika mikataba wasiruhusiwe kupewa kazi yoyote. “Mkandarasi
huyu na wengine ambao hawajakamilisha miradi hii ambayo ilipaswa ikamilike
mwezi Februari wasiruhusiwe kupewa kazi yoyote hata ya shilingi 500. Hatuwezi
kuwa na watu ambao hawawezi kuona fikra za Rais wetu anatafuta fedha, analeta
fedha, na bado wanakuwa goigoi hatuwezi kukubali hata kidogo. Maelekezo yangu
kwa Mkandarasi huyu na wengine wa aina hii wasiruhusuiwe kufanya a kazi kokote
ndani ya TARURA” aliagiza Mchengerwa.
Aidha,
alitoa maelekezo mahususi kwa Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Mkuu wa Wilaya na
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma kuweka utaratibu mzuri wa watu wa kuingia na kutoka katika
Stesheni ya reli ya mwendokasi (SGR), Samia Suluhu Hassan, Dodoma, kwa sababu Jiji la Dodoma ndio makao makuu ya
nchi.
“Ninawataka
wakurugenzi wote wa majiji lakini hasa Jiji la Dodoma ambalo ndio makao makuu
ya nchi, Mkuu wa Mkoa na Mkuu wa wilaya nendeni mkajipange hasa pale eneo la Stesheni
ya reli, utaratibu wa watu kuingia na kutoka haujakaa vizuri, makakae pamoja na
TRC muweke utaratibu mzuri. Haieleweki na Rais wetu hawezi kutuelewa, yeye
ameleta fedha, ninyi wajibu wenu ni kuwasaidia watanzania ili waweze kupata
njia nzuri ya kuingia kwenye Stesheni ya reli. Sasa ninawataka ninyi na TARURA mkajipange
vizuri, mkazungumzeni na wizara ya uchukuzi ili kuweka utaratibu watanzania
wanaokwenda na kurudi kutoka Dodoma waweze kuingia na kupita vizuri eneo lile”
alisema Mchengerwa.
Kwa
upande wake Diwani wa Kata Ya Makole, Omar Omar, alimshukuru Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Rais Tawala za Mkioa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kwa mikakati
mizuri ya kuboresha miundombinu ya Jiji la Dodoma na kukemea wakandarasi wote
ambao hawatekelezi miradi yao kwa wakati. Aidha, alitoa wito kwa wakandarasi
kusimamia na kutekeleza miradi kwa wakati.
“Tumeona
namna alivyokuwa anazungumza, kuonesha ukali namna ambavyo atataka kustawisha
makao makuu ya nchi Dodoma, hususani katika suala la maendeleo na upangiliaji wa mji wa Dodoma nampongeza
pia kwakuwa amekuwa mkali kwa wakandarasi wavivu ambao wanapewa kazi na
kutoweza kutekeleza kwa wakati. Rai yangu ninawasisitiza wakandarasi wote ambao
wamepewa agizo hili waweze kufanya kazi zao kwa wakati na miradi kutekelezeka
kwa wakati” alitoa rai Omar.
Nae
mfanyabiashara wa Soko Kuu la Majengo, Samiri Majid , aliunga mkono agizo la
waziri Mchengerwa la kuwasimamisha wakandarasi wasiotekeleza miradi yao kwa
wakati na akatoa rai yake kwa wakandarasi wote na kusisitiza watangulize
uzalendo mbele badala ya maslahi yao binafsi.
“kwa
upande wangu nianaona jambo hilo ni jema kwasababu wakandarasi wa namna hiyo
wanachelewesha sana maendeleo ya taifa letu. Rai yangu kwa wakandarasi ni
kwamba wakati wakikabidhiwa ‘share’ ya mradi wajitahidi kufanya kazi hiyo kama
walivyokuwa wanahitaji kupewa kufanya hiyo kazi, kwasababu mkandarasi
atakapokuwa anahitaji kupata ‘share’ atatumia mbinu yoyote ile kuhakikisha
anapata. Hivyo niwaombe watangulize uzalendo mbele, maslahi ya nchi mbele na
wasitangulize maslahi yao binafsi ili taifa letu lizidi kukua na kuwa taifa
linalojengeka kadri siku zinavyokwenda” alisema Majid.
MWISHO
Comments
Post a Comment