Miundombinu ni nyenzo ya maendeleo ya Jiji la Dodoma
Na. Shahanazi Subeti, DODOMA
Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa
na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) pamoja na
Halmashauri ya Jiji la Dodoma zilisaini mkataba wa TACTIC wenye thamani ya shilingi Bilioni 14.2 kwa
lengo la kuboresha miundombinu, kuimarisha usimamizi wa uendelezaji miji na
kuboresha mazingira ya uwekezaji ili kukuza uchumi wa halmashauri ya jiji.
Hafla hiyo ya Utiaji saini
ilifanyika bustani ya Chinangali Park jijini Dodoma katika hafla ya utiaji
saini mkataba wa ujenzi wa soko kuu la majengo pamoja na ujenzi wa kituo cha
daladala eneo la Mshikamano, Kizota na Nzuguni.
Akielezea tukio hilo Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za
Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mohamed Mchengerwa alisema, mikataba hii
itakwenda kuleta mapinduzi makubwa ya kiuchumi kwa watanzania wanaoishi Dodoma na
aliwaomba wakandarasi kutekeleza majukumu yao kwa wakati. "Tunapoboresha
miundombinu hii itawafanya watanzania na wafanyabiashara, kuweza kusogeza
biashara zao karibu, kuweza kutumia vivuko, madaraja na barabara ambazo
tumekwisha saini hapa, matarajio yetu usimamizi wa miradi hii kwa kila mmoja
wetu anajukumu la kuitunza kwa sababu gharama inayotumika ni kubwa sana. Nina muelekeza
Mkandarasi ambae tumesaini leo mkataba nenda kafanye kazi usiku na mchana ili
kukamilisha muda uliopangwa na hakutakuwa na nyongeza ya muda" alisema Mchengerwa
Sambamba na hilo, alimpongeza Rais kwa kuweza kulijenga jiji "ameyafanya
mengi ndani ya muda mfupi na sisi wasaidizi wake wa karibu kuna wakati tunajiuliza
fedha hizi zinatoka wapi, miaka 10 iliyopita
hatukuwa na barabara za lami wala majengo makubwa makubwa, tulianza na
ujenzi wa Ofisi za serikali lakini Rais akaamua kujenga maghorofa katika mji wa serikali na sasa
akaona upo umuhimu wa kwenda kuboresha majiji na miji, akatafuta fedha
akatuelekeza wasaidizi wake kuhakikisha tunakwenda kuzisimamia ili Dodoma iwe makao makuu
ya nchi yetu" alisema Mchengerwa
Pia aliwataka wananchi wa Dodoma kumpongeza sana Mbunge wao
kwa kazi kubwa anayoifanya kwa kutatua kero katika mitaa yao "kila mmoja
unaemsikia hapa amezungumza Kwa kina na aliwazungumzia wananchi wake amegusa
kila kata na amesema kuhusu changamoto kadhaa ambazo madiwani wa nchi wanakutana
nazo hasa madiwani wa Dodoma na nimepokea changamoto hizi na kwakuwa kwenye
wizara hii Rais mwenyewe nitaziwasilisha kwake" alisema Mchengerwa.
Kwa upande wake wakala wa Barabara za mijini na vijijini (
TARURA) mhandisi Victor Seif alisema
Halmashauri ya Jiji la Dodoma, awamu ya kwanza kazi zinazofanyika ni ujenzi wa
Barabara za mijini katika ( Km 13.0) na ujenzi wa jengo la usimamizi na uratibu
wa miradi pia katika awamu ya pili kazi
zinazofanyika katika mkataba ni pamoja na uboreshaji wa Soko Kuu la Majengo, kituo
Cha daladala eneo la Mshikamano, uboreshaji wa stendi ya mabasi madogo eneo la
Kizota, ujenzi wa stendi ya mabasi madogo eneo la Nzuguni, ujenzi wa vivuko
maji(footbridges) katika maeneo ya Chaduru, Maili mbili na Ntyuka.
Alisema kuwa miradi hiyo
kwa awamu zote mbili unasimamiwa
na mshauri elekezi ambae ni M/S Hong- IK Engineering consultants CO.ltd
in association with gauge pro consult(T) ltd.and G and Y engineering consult PLC, kwa gharama ya mkataba wa usimamizi
ni Milioni 667,100,000.00 "katika hatua ya utekelezaji awamu ya kwanza mradi umefikia asilimia 37.7
ya utekelezaji ( malengo ya utekelezaji ni kufikia asilimia 88.6 Mpaka mwisho wa
mwezi Desemba, 2024 hivyo mkandarasi wa ‘package 1’ yupo nyuma kwa asilimia
59.9. Kwa awamu ya pili ni kuanza utekelezaji tarehe 1/2/2025 kwa mkataba wa
miezi 12. Pia utekelezaji unafuata mpango wa manunuzi ulioidhinishwa katika
andiko la mradi ‘project appraisal document’ pamoja na makubaliano ya
utekelezaji ‘financing agreement’ kati ya serikali kuu na Benki ya Dunia"
alisema Seif.
Kwa upande wake, Mbunge wa Dodoma,
Anthony Mavunde, alisema kuwa miradi hii imeleta mageuzi na mapinduzi sana kwa kuleta maendeleo katika Halmashauri ya
Jiji la Dodoma" naishukuru sana serikali kwa mradi ambao leo tunakwenda
kutia saini mradi ambao una thamani
zaidi ya shilingi Bilioni 24.0 ukiwa ni awamu ya kwanza ya mradi wa
kundi la kwanza ‘tier 1’ ambapo tunaamini kabisa kupitia miradi huu tutakwenda kuleta mapinduzi
makubwa ya kusaidia kutatua changamoto
za miundombinu ndani ya Jiji letu la
Dodoma na hii ni awamu ya pili ambayo
tunasaini leo una thamani ya Bilioni 14.2 mradi huu unaenda kufanya yafuatayo
kuboresha Soko Kuu la Majengo pamoja na kituo cha daladala eneo la Mshikamano, uboreshaji wa stendi ya mabasi
madogo eneo la Kizota, ujenzi wa stendi ya mabasi madogo eneo la Nzuguni na
ujenzi wa vivuko maji (footbridges) katika maeneo ya Chaduru, Mailimbili na Ntyuka"
alisema Mavunde.
Pia aliongezea Kwa kumshukuru
Raisi wa jamhuri ya muungano wa Tanzania
Dkt. Samia Suluhu Hassan Kwa kuwezesha Dodoma kuwa na miradi mikubwa ya
kimaendeleo na kufanya iendelee kunga'ra zaidi "Dodoma tumepata upendeleo
wa kipekee wa kuwa na miradi mingi
,miaka 20 iliyopita Dodoma katikati eneo ambalo lilikuwa na kiwango cha lami
ilikuwa ni ‘full street’ kuna wakati kulikuwa na shida kidogo leo ukizunguka
katika Jiji la Dodoma katikati, eneo
kubwa limezungukwa na Barabara yenye kiwango cha lami katika halmashauri zote
nchi nzima, Jiji la Dodoma ndio linaongoza kwa mtandao mrefu wa Barabara za
kiwango cha lami, sisi tuna Kilomita 249.12 hivyo Jiji la Dodoma ndio kinara kwa
Tanzania nzima, nashukuru sana kwa kazi kubwa iliyofanyika kupitia miradi
mbalimbali" alisema Mavunde
Nae Mkuu wa Mkoa wa Dodoma
Rosemary Senyamule, alisema kuwa amefurahishwa sana na utiaji saini huo kwasababu
ni jambo ambalo sio la kawaida na husaidia kutatua changamoto za wananchi wa
Jiji la Dodoma."Nipo hapa kushudia mkataba kwa ajili ya ujenzi wa miradi
mikubwa ya kimkakati kwa Jiji la Dodoma haya mambo ni ya kushangaza lakini
Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ndiye Rais anaeyafanya haya" alisema
Senyamule.
MWISHO.
Comments
Post a Comment