Wananchi washuhudia utiaji saini mkataba wa mradi wa TACTIC
Na. Coletha Charles, DODOMA
Wananchi wa Jiji la Dodoma
wamejitokeza kwa wingi kushuhudia hafla ya utiaji saini mkataba wa Mradi wa “Tanzania Cities Transforming Infrastructure
and Competitiveness” (TACTIC), unaolenga kuboresha na kujenga miundombinu
muhimu katika jiji hilo ikiwa ni pamoja na Uboreshaji wa Ujenzi wa Soko, Vituo
vya daladala pamoja na vivuko.
Hafla hiyo, iliyofanyika
katika viwanja vya Chinangali, inahusisha uboreshaji wa Soko Kuu la Majengo,
Kituo cha Daladala Mshikamano, Stendi ya mabasi madogo eneo la Kizota, ujenzi
wa stendi ya mabasi madogo eneo la Nzuguni, pamoja na ujenzi wa vivuko katika
maeneo ya Chadulu, Mailimbili, na Ntyuka.
Akizungumza wakati wa hafla
hiyo, Mgeni Rasmi ambaye ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Mohamed
Mchengerwa (Mb), aliwaomba watanzania kuitunza miradi hiyo inayotekelezwa
kwenye majiji na miji zaidi ya 45 kwasababu ina thamani kubwa zaidi ya Trilioni
1.1.
Alisema kuwa mkataba huo wa
bilioni 14.2 wa kuboresha na kujenga miradi ni matarajio ya kila mwanadodoma
kuwa utaleta mapinduzi makubwa kiuchumi kwa watanzania na kuitunza miundombinu.
“Ninawaomba watanzania simamieni miradi hii, ilikusudi iweze kuwasaidia
watanzania wa karne hii na karne zinazokuja. Mnapoona wakandarasi wanalegalega
tupeni taarifa, tuchukue hatua kwasababu miradi hii, Dkt. Samia Suluhu Hassan
amewakusudia watanzania, sasa haiwezekani fedha hizi zote zitolewe na miradi
itekelezwe kwa kiwango cha chini. Tumeshuhudia tukio la utiajia saini wa sehemu
ya pili ya utekelezaji wa miradi, matarajio yetu usimamizi uwe wa kina” alisema
Mchengerwa.
Aidha, Mchengerwa
aliwaelekeza watendaji wa serikali chini ya TAMISEMI wasimamie miradi hiyo,
wakipita sehemu wakakuta kuna changamoto ambazo watendaji hao walikuwa na uwezo
wa kuzitatua watachukua hatua kwasababu jukumu kubwa ni kuitunza miundombinu
inayojengwa.
Kwa upande wake,
mfanyabiashara na mkazi wa Nzuguni, Kuruthum
Musse, alieleza
furaha yake kubwa baada ya serikali kuwapelekea mradi wa ujenzi wa kituo cha
daladala katika eneo lao kwa kuwa ujenzi huo ni hatua muhimu katika kuboresha
huduma za usafiri na kupunguza changamoto kwa wananchi, kushushwa
sehemu ambayo mazingira siyo rafiki.
“Miundombinu tunayoenda kutengenezewa
tunatakiwa tuitunze, tuiangalie, pia tuilinde hata ukiona mtu anataka kufanya
chochote kwenye huo mradi lazima ukemee na unajua serikali ni mimi na wewe. Kituo hiki kitawasaidia abiria kupata usafiri
kwa urahisi na kwa wakati. Naona matumaini makubwa kuwa mradi huu utaleta
mabadiliko chanya katika maisha ya watu.”
alisema Musse.
Nae, Mwanafunzi anayesoma
stashahada ya Utendaji katika Chuo cha Serikali za Mitaa Dodoma, Kampasi ya
Dodoma Mjini, Jafar Jamal, aliipongeza serikali kwa hatua waliyoichukua ya
kusaini mkataba kwa sababu wananchi watanufaika na miradi hiyo itaondoa
changamoto nyingi za usafiri kwenye maeneo yenye wingi wa abiria. “Binafsi kama
mwananchi nitajitahidi kulinda miundombinu inayotekelezwa na serikali ili ilete
manufaa kwetu. Lakini pia hii ni hatua muhimu kwa sisi wakazi wa Dodoma
kwasababu tunahitaji miundombinu bora ili kuboresha maisha. Kwangu mimi
natarajia kuona mabadiliko makubwa kwenye huduma za usafiri” alisema Jamal.
Mradi wa TACTIC ni mojawapo
ya miradi inayofadhiliwa na serikali kuu kupitia mkopo wa Benki ya Dunia wenye
thamani ya Dola za Kimarekani Milioni 410 (Bila VAT). Malengo ya mradi huu ni
kuboresha miundombinu ya Tanzania Pamoja na kuzijengea uwezo taasisi
(Halmashauri) ili ziweze kujiimarisha katika usimamizi wa uendeshaji miji pamoja
na ukusanyaji wa mapato.
MWISHO
Comments
Post a Comment