Wasimamizi wa Mikopo Halmashauri Wapewa Mafunzo
Na. Coletha Charles, DODOMA
Kamati ya huduma ya Mikopo ya Wanawake, Vijana na watu wenye
Ulemavu ngazi ya halmashauri wamepewa mafunzo ya kuhakiki, kutathimini, sheria
na kanuni za utoaji wa mkopo ili kuwajengea uwezo wa usimamizi wa mikopo hiyo.
Mafunzo hayo yalitolewa katika Ofisi ya Mkuu wa Divisheni ya
Maendeleo ya Jamii, Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa lengo la kutoa muongozo
wa utoaji na usimamizi wa mikopo kwa wasimamizi hao. Mkuu wa Divisheni ya
Maendeleo ya Jamii, Charity Sichona alisema kulingana na kanuni mpya za mwaka
2024 wameweka ratiba ya kufanya tathimini ya maombi ya kikundi kwa kuweka
kumbukumbu.
Alisema katika ngazi ya kata wasimamizi wameendelea kutoa
mafunzo na kusajili vikundi. Alisema kuwa takribani vikundi 1,000 vimejisajili na
hatua ya kuomba mkopo inaendelea kwa kuangalia tathimini ya miradi ya
wanakikundi. “Mafunzo kama haya tulishatoa katika ngazi mbalimbali hasa kata
ambapo wanajukumu kubwa la kuchakata maombi hayo na kuwapatia mafunzo
wanakikundi hadi hatua ya kupata mikopo. Lakini pia mafunzo kama haya yanaweza
kujenga uelewa mpana zaidi kwa viongozi ngazi ya halmashauri” alisema Sichona.
Mwezeshaji wa Mafunzo, Daniel Mpangwa alisema kuwa mikopo
hiyo itatolewa kwa makundi ambapo wanawake kuanzia watu wa tano 40%, vijana
kuanzia wa tano 40% na watu wenye ulemavu 20% kuanzia watu wawili au mmoja.
Alisema kuwa wasimamizi wanatakiwa kuzingatia mfumo jumuishi
na mfumo wa serikali ulioboresha kwa maelekezo kama utoaji wa mikopo kwa
utaratibu wa taasisi za fedha, majukumu ya taasisi ya fedha na mamlaka ya
serikali za mitaa, tathimini na uboreshaji, mikopo ya vifaa, ushirikiano na
wadau mbalimbali na kuepuka mgongano wa kimaslahi. “Naamini kamati hii ikitoka
hapa itaenda kufanya kazi vizuri na kwa weledi. Lakini, mafunzo haya yameweza
kutolewa ngazi nyingine za kamati za maendeleo za kata ambayo tayari
yamekwishafanyika lakini pia kwa Afisa Maendeleo Kata ambapo sasa michakato ya
mikopo bado inaendelea” alisema Mpangwa.
Mratibu wa Mikopo ya asilimia 10 Halmashauri ya Jiji la
Dodoma, Hidaya Mizega alisema kwa mujibu wa sheria ya utengaji wa fedha za
mikopo, Mamlaka za Serikali za Mitaa zitazingatia uwiano wa 4:4:2 wa waombaji
wote wa mkopo bila ya kumpendelea yeyote.Serikali za Mitaa zitaruhusiwa
kuhamisha fedha na kutumika katika kundi lingine lenye uhitaji kulingana na
wingi wa watu kwa maelezo juu ya wajibu wa mamlaka ya utengaji, utoaji na
urejeshaji wa mikopo, aliongeza.
Viwango vya ukomo wa utoaji wa mikopo midogo ni shilingi
500,000 kiwango cha chini na kiwango cha juu ni shilingi 9,999,999. Mkopo wa
kati kiwango cha chini ni shilingi 10,000,000 na kiwango cha juu ni shilingi
49,999,999 na mkopo mkubwa kiwango cha chini ni shilingi 50,000,000 na kiwango
cha juu ni shilingi 150,000,000.
MWISHO
Comments
Post a Comment