Jamii imeaswa isifumbie macho Ukatili wa Kijinsia
Na. Faraja Mbise, DODOMA
Jamii
imeaswa kutoyafumbia macho masuala ya ukatili wa kijinsia na kutakiwa kuripoti
kwenye vyombo vya sheria matukio ya ubakaji, ulawiti na ndoa za utotoni.
Mamia ya wanafunzi waliojitokeza
Hayo,
yalisemwa na Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Ng’hongh’onha, Patrick Mwachambi ambaye
ni muwakilishi wa mgeni rasmi, alipokuwa akizungumza na wananchi waliojitokeza
katika Uzinduzi wa Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia ngazi ya Halmashauri
ya Jiji la Dodoma katika Kata ya Ng’hong’onha.
“Natoa
wito kwa wananchi wenzangu, kuwatumia ipasavyo wataalam wetu kwasababu wako
tayari wakati wote kuhakikisha kuwa vitendo vya ukatili vinakomeshwa na
wahusika wanachukuliwa hatua za kisheria. Namshukuru sana Mkurugenzi wa Jiji la
Dodoma, tumejifunza mengi kupitia wataalam. Kwahiyo, nawaomba wananchi
tuzingatie elimu tuliyopewa na kuahidi kuifanyia kazi, yote yaliyoelekezwa
tutayatekeleza bila kuathiri taratibu za kisheria” alisisitiza Mwachambi.
Akizungumzia
kampeni ya mwaka huu isemayo “Kuelekea miaka 30 ya Beijing: CHAGUA
Kutokomeza Ukatili wa Kijinsia” mgeni rasmi alitoa historia fupi
kuhusiana na harakati za kupambana na kutokomeza ukatili wa kijinsia kwa
wanawake na watoto.
“Kaulimbiu
hii inaendelea kusisitiza kuendeleza mapambano dhidi ya ukatili yaliyoanza
miaka mingi nyuma na kutiliwa mkazo na Mkutano wa Beijing wa mwaka 1995 ambao
ni mkutuno wanne wa Dunia kwa wanawake uliofanyika Beijing nchini China.
Mkutano huu uliwakutanisha kwa pamoja serikali za mataifa mbalimbali pamoja na
wanaharakati, na uliwezesha kuundwa kwa jukwaa la kuchukua hatua la Beijing, na
agenda ya msingi ya haki za wanawake katika ngazi za kimataifa ambao kati ya
malengo yake makubwa ni kutokomeza ukatili wa kijinsia na kusisitiza
upatikanaji wa haki za wanawake katika nyanja zote za kimataifa na kutetea haki
za kijinsia” alisema Mwachambi.
Afisa Maendeleo ya Jamii ambae ni Mratibu wa Jinsia na Watoto Jiji la Dodoma, Fatuma Daudi akisisitiza jambo
Kwa
upande wake Afisa Maendeleo ya Jamii ambae ni Mratibu wa Jinsia na Watoto Jiji
la Dodoma, Fatuma Daudi, alizungumzia mlolongo wa matukio mbalimbali ambayo
yanaadhimishwa ndani ya siku 16 za kupinga Ukatili wa Kijinsia. Daudi alisema “tukiwa
tupo katika kampeni za siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia, kampeni hizi
zinatokana na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Kimataifa Kofi Annan ambaye
aliona vitendo vya ukatili wa kijinsia unazidi
hivyo kitengwe kipindi maalum cha kufanya kampeni ili kukomesha vitendo
vya ukatili wa kijinsia. Kipindi kilichaguliwa kuanza tarehe 25 Novemba na kuisha
tarehe10 ya mwezi Desemba, ukizihesabu siku hizi zinafika siku 16, ndani ya
siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia kuna siku mbalimbali zenye matukio
maalum kati ya hizo kuna siku ya Novemba 25, ambayo ni siku ya kupinga ukatili
na unyanyasaji dhidi ya wanawake, Novemba 29, ambayo ni siku ya kimataifa ya utetezi wa haki za
wanawake, Desemba moja ambayo ni siku ya UKIMWI Duniani, Desemba 05, siku ya
kujitolea Duniani na siku hizi zinahitimishwa na tarehe 10 Desemba, ambayo ni
siku ya Kimataifa ya Haki za Binadamu. Siku hizi zote zipo ili kuhakikisha wanawake,
watoto na Jamii kwa ujumla inaepukana na vitendo vya ukatili”.
Kuhusu
msaada wa kisheria unaopatiwa kwa wahanga wa ukatili wa kijinsia, Afisa
Maendeleo ya Jamii, Dawati la Msaada wa Kisheria katika Halmashauri ya Jiji la
Dodoma, Frida Ngowi aliogelea umuhimu wa dawati la sheria katika kupambana na
masuala ya ukatili wa kijinsia.
“Dawati
hili la msaada wa kisheria lipo kwa ajili ya kutoa elimu ili watu tufahamu haki
zetu, pili dawati hili linawasaidia watu kupata huduma za msaada wa kisheria
ambapo kuna makundi maalumu, kundi la kwanza ni wanawake, watoto, walemavu na
wazee lakini pia mwananchi yeyote ambaye hana uwezo wa kumudu gharama za
mahakama. Kwahiyo, huduma tunazotoa ni pamoja na ukatili wa kijinsia unaotendeka
kwa wanawake, watoto na wanaume pia wanaopitia changamoto za ukatili wa
kijinsia” alisisitiza Ngowi.
Vilevile,
Afisa Ustawi wa Jamii Mwanadamizi Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Aneth Mwambya aliwasisitiza
watoto kutoa taarifa kwa wazazi, dawati la kijinsia au kwa walimu endapo watakutana
na vitendo hivyo viovu vya ukatili wa kijinsia. “Ukatili wa ngono au kingoni,
tunauona, tunaenda likizo, takwimu zinasema asilimia 60 ya ukatili unafanyika nyumbani,
unapofanyiwa kitendo chochote ambacho si kwa ridhaa yako kwa maana unapata
madhara kiakili, kimwili na kingono unatakiwa utoe taarifa kwa wazazi, jirani
kama unamwamini, dawati la jinsia, kituo cha polisi na serikali za mitaa”
alisisitiza Mwambya.
Nae
Mwanafunzi wa Shule ya Msingi ya Ng’hong’onha, Theresia Samson alitoa rai kwa
watoto wanaopitia ukatili wa kijinsia majumbani kwao, waweze kuripoti matukio
hayo ili kupunguza idadi ya matukio ya ukatili wa kijinsia. “Mimi nimeigiza
kama mtoto niliyebakwa na mjomba, nawashauri watoto wengine wanaofanyiwa
vitendo hivi wasikae kimya wakatoe taarifa kwa walimu, watu wanaowaamini au kwa
wazazi wao” alishauri Samson.
MWISHO
Comments
Post a Comment