Kata ya Chamwino kipaumbele Lishe shuleni
Na.
Dennis Gondwe, CHAMWINO
KATA
ya Chamwino imetoa kupaumbele katika agenda ya lishe ili kuhakikisha wanafunzi
wanakuwa na lishe bora na kuendelea na masomo yao vizuri.
![]() |
Afisa Mtendaji wa Kata ya Chamwino, Lucas Nkelege akiongelea umuhimu wa Lishe shuleni |
Kauli
hiyo ilitolewa na Afisa Mtendaji wa Kata ya Chamwino, Lucas Nkelege alipokuwa
akiongea na walimu, wanafunzi na wadau wa masuala ya lishe katika Shule ya Msingi
Chamwino iliyopo katika Kata ya Chamwino, Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
“Leo
ni maadhimisho ya kidunia kuhamaisha matumizi ya mimea jamii ya mikunde. Kama
maharage, njegere, choroko, mbaazi. Sisi Kata ya Chamwino suala la lishe lina
umuhimu mkubwa sana. Lengo ni kupinga hali ya udumavu, ukondefu na athari zote
zinazotokana na lishe duni. Kata ya Chamwino tumeweka mikakati mizuri kuhakikisha
wanafunzi katika shule zetu tatu za msingi na moja ya sekondari wanaweza kupata
chakula shuleni. Na leo hapa tumekuja Shule ya Msingi Chamwino yenye wanafunzi
takribani 2,500 kuhamasisha lishe. Na hii shule inafanya vizuri katika utoaji
wa chakula shuleni, inafikia asilimia 92. Shule inatoa uji kwa madarasa ya
awali na chakula cha mchana kuanzia darasa la tatu hadi la saba” alisema
Nkelege.
Mkurugenzi
wa Idara ya Usalama wa Chakula kutoka Wizara ya Kilimo, Dkt. Honest Kessy
alisema kuwa maadhimisho ya siku ya kula mazao ya mikunde kuna lenga
kuhamasisha ulaji wa vyakula vyenye virutubishi mwilini. “Wanafunzi mpende kula
maharage na muwashawishi wazazi waweze kuwapikia maharage na mboga jamii ya
mikunde. Vyote hivi vyakula vinaumuhimu sana kwa sababu vinatuongezea
virutubishi katika miili yetu, vinaongeza uwezo wetu wa kufikiri na kuelewa
darasani. Niwaombe sana tusipuuze vyakula vinayotokana na jamii ya mikunde”
alisema Dkt. Kessy.
![]() |
Mkurugenzi wa Idara ya Usalama wa Chakula kutoka Wizara ya Kilimo, Dkt. Honest Kessy |
Akitoa
shukrani kwa niaba ya Shule ya Msingi Chamwino, Mwl. Ezekiel Lenjima alisema
kuwa shule hiyo imefurahia zoezi la upandaji wa mbogamboga. “Kwa niaba ya Shule
ya Msingi Chamwisho niwashukuru viongozi wa serikali, sekta binafsi na
waendesha baiskeli kufanya kilele cha maadhimisho haya katika shule yetu. Tuwahakikishie
kwamba mbegu hizi za mboga tulizopanda shuleni hapa tutazitunza, tutazimwagilia
na mavuno yake yatatusaidia sana katika kuchanganya mboga kwenye maharage.
Maharage tunayotumia kwa chakula katika shule yetu yatakuwa yameongezewa virutubishi
vitakavyoongeza lishe kwa wananfunzi wetu na kukuza uwezo wao wa kiakili”
alisema Lenjima.
Zoezi
la kusia mbegu za mboga katika Shule ya Msingi Chamwino lilitanguliwa na mbio
za baiskeli zilizolenga kuhamaisha afya bora dhidi ya magonjwa yasiyo ya
kuambuza na kuchochea masuala ya lishe bora kwa jamii.
MWISHO
Comments
Post a Comment