Wanafunzi Dodoma watakiwa kutoa taarifa za ukatili wa kijinsia
Na. Dennis Gondwe, CHAMWINO
WANAFUNZI
wa shule za msingi mkoani Dodoma wametakiwa kutoa taarifa kwa Dawati la Jinsia
na Watoto pindi watakapofanyiwa ukatili wa kijinsia ili kuwa na jamii isiyo na
ukatili wa kijinsia.
![]() |
Mkaguzi wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma, Theresia Mdendemi akiongea na wanafunzi |
Kauli
hiyo ilitolewa na Mkaguzi wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma, Theresia Mdendemi, kutoka Dawati la Jinsia na Watoto
Mkoa wa Dodoma alipokuwa akiongea na wanafunzi wa Shule ya Msingi Chamwino
katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Insp.
Mdendemi alisema “watoto wazuri msisite kutoa taarifa kwa Dawati la Jinsia na
Watoto katika Jeshi la Polisi na watu mnaowaamini pindi mnapofanyiwa ukatili wa
kijinsia. Hakikisha ndani ya saa 72 mmetoa taarifa kwenye Dawati la Jinsia na
Watoto au mtu mnaemwamini ili tuweze kupata Ushahidi. Mtuhumiwa tunatakiwa
tumuunganishe kosa alilofanya na ushahidi tutakaopata toka kwenye mwili wako”.
Alisema
kuwa mara nyingi ukatili umekuwa ukifanyika kwa watu wa karibu jambo
linalofanya mara nyingi matukio hayo kutoripotiwa. “Kwa hiyo tunatoa rai, awe
baba au mama, awe shangazi au mjomba, awe mama wakufikia au baba wakufikia,
amefanya ukatili toa taarifa mapema ili tuweze kulishughulikia” alisisitiza.
Alisema
kuwa kutoa taarifa mapema kutawawezesha kuwaepusha watoto waliofanyiwa ukatili
na magonjwa yanayoambuliza. “Unapotoa taarifa mapema unatoa mwanya kwa sisi
kuweza kukusaidia wewe usipate magonjwa yanayoambukiza mfano maambukizi ya
virusi vyua ukimwi, mimba zisizotarajiwa na magonjwa ya zinaa. Naimani kwa
ujumbe huu mtakuwa mpo tayari kushirikiana na dawati la jinsia kwa kutoa
taarifa sahihi, hata kama haumfahamu jina aliyekufanyia ukatili ila ukamtaja
kwa muonekano kwa mfano alionekana ni mweupe, ana masharubu, anaongea rafuzi
flani, huo ndio utoaji taarifa sahihi. Lakini mnapokuwa barabarani mmekuwa
mkifanyiwa ukatili, angalia rangi ya gari, muonekano wa gari pia shika namba za
gari” alisema Mkaguzi wa Polisi Mdendemi.
Kwa
upande wake, Cpl. Edith Siwango kutoka Dawati la Jinsia na Watoto wa Jeshi la
Polisi Wilaya ya Dodoma aliwataka wazazi kutenga muda kuzungumza na watoto wao.
“Tupo hapa kwa ajili ya kuwalinda watoto wetu. Wazazi mlio hapa nawaomba mtenge
muda wa kuzungumza na watoto wenu ili wawe wanaelewa. Kuwachapa watoto siyo
suluhisho, kuongea nao na kuwaelimisha ndiyo suluhu. Kumuelekeza mtoto ndiyo
suluhu kwa maisha ya sasa. Kama unataka mtoto wako awe msikivu ongea nae,
tusiwaachie walimu peke yao, tukiongea nao watatueleza changamoto zao” alisema
Cpl. Siwango.
![]() |
Cpl. Edith Siwango kutoka Dawati la Jinsia na Watoto wa Jeshi la Polisi Wilaya ya Dodoma |
MWISHO
Comments
Post a Comment