Wazazi Chamwino washauriwa kutenga muda kuzungumza na watoto

 Na. Dennis Gondwe, CHAMWINO

WAZAZI na walezi katika Wilaya ya Dodoma wameshauriwa kutenga muda wa kukaa na kuongea na watoto wao ili waweze kubaini changamoto zinazowakabili ikiwemo kufanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia.

Cpl. Edith Siwango kutoka Dawati la Jinsia na Watoto wa Jeshi la Polisi Wilaya ya Dodoma alipokuwa akiongea na wanafunzi, walimu na wadau wa Lishe katika Shule ya Msingi Chamwino


Ushauri huo ulitolewa na Cpl. Edith Siwango kutoka Dawati la Jinsia na Watoto wa Jeshi la Polisi Wilaya ya Dodoma alipokuwa akiongea na wanafunzi, walimu na wadau wa masuala ya Lishe katika Shule ya Msingi Chamwino iliyopo Kata ya Chamwino Halmashauri ya Jiji la Dodoma.

Cpl. Siwango alisema “tupo hapa kwa ajili ya kuwalinda watoto wetu. Wazazi na walezi mlio hapa nawaomba mtenge muda wa kuzungumza na watoto wenu. Mazungumzo hayo yatawasaidia kuwaelewa watoto wenu. Watoto wamekuwa wakipitia changamoto mbalimbali zinazohusisha ukatili wa kijinsia na kushindwa kuwaeleza wazazi na walezi kwa sababu hawana muda wa kukaa na kuwasilikiza watoto. Matokeo yake mtoto anafanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa muda mrefu na kumsababishia madhara. Baadhi ya wazazi wamekuwa na tabia ya kuwachapa watoto kupitiliza. Kuwachapa watoto siyo suluhisho, kuongea nao na kuwaelimisha ndiyo suluhu. Kumuelekeza mtoto ndiyo suluhu kwa maisha ya sasa. Kama unataka mtoto wako awe msikivu ongea nae, tusiwaachie walimu peke yao, tukiongea nao watatueleza changamoto zao hasa masuala ya vitendo vya ukatili wa kijinsia” alisema Cpl. Siwango.

Aidha, aliwataka watoto kuwa wasikivu na kufuata yale wanayoelekezwa na wazazi na walimu ili waweze kuwa raia wema. “Napenda kuongea nanyi wanafunzi, mnatakiwa kuwa wasikivu na wenye adabu kwa walimu, wazazi na jamii inayowazunguka. Mnapoelekezwa au kukatazwa jambo kwa manufaa yenu mnatakiwa kusikiliza. Watoto wenye adabu na heshima hata kwenye masomo yao hufanya vizuri na kufaulu na kila mtu anampenda mtoto mwenye adabu na heshima” alisema Cpl. Siwango.

Akiongelea suala la Lishe, aliwashauri wanafunzi kuzingatia mafundisho ya lishe wanayopewa shuleni. “Leo tupo hapa kwa ajili ya kuhamasisha mazoezi na lishe bora, ni vizuri mkazingatia masuala ya lishe hasa kilimo cha bustani ya mbogamboga ili zitumike kwa ajili ya mboga na kuboresha hali ya lishe katika jamii. Nendeni mkalime bustani za mbogamboga nyumbani ili kujihakikishia lishe bora” alisema Cpl. Siwango.

Zoezi la kusia mbegu za mboga katika Shule ya Msingi Chamwino lilitanguliwa na mbio za baiskeli zilizolenga kuhamaisha afya bora dhidi ya magonjwa yasiyo ya kuambuza na kuchochea masuala ya lishe bora kwa jamii.



MWISHO

Comments

Popular Posts

Wananchi Makutupora wafunguka changamoto ya Maji, Umeme na Shule kwa Mkuu wa Mkoa

Waziri Mchengerwa apongeza usimamizi wa miradi jijini Dodoma

Mkataba ujenzi Uwanja wa Mpira wa Miguu wasainiwa Dodoma