CCM CHANG’OMBE YAMPONGEZA DIWANI FUNDIKILA KUBORESHA HUDUMA ZA JAMII

Na. Dennis Gondwe, CHANG’OMBE

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Chang’ombe kimempongeza Diwani wa kata hiyo Bakari Fundikila kwa kuhakikisha huduma za kijamii zinawafikia wananchi ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Kituo cha Afya Chang’ombe.

Wananchi wakifuatilia mkutano wa hadhara


Pongezi hizo zilitolewa na Mwenyekiti wa CCM Kata ya Chang’ombe, Bashir Iddy katika mkutano wa hadhara uliofanyika Ofisi ya Serikali ya Mtaa wa Hamvi jijini Dodoma.

Iddy alisema kuwa Kata ya Chang’ombe inapiga hatua ya maendeleo kwa kasi kutokana na Diwani wake kusimamia maendeleo. “Maendeleo haya tunayoyaona ni baada ya Diwani kusimama na kuizungumzia na kuitetea Chang’ombe. Mheshimiwa Diwani umekwenda kufanya harakati za namna gani wananchi wa Kata ya Chang’ombe wanaenda kupata huduma bora za kijamii. Leo tumekuwa na Kituo cha Afya Chang’ombe ambacho ni kituo cha mfano kwa ubora wa majengo, ukubwa wa eneo na huduma. Pale kuna jengo la mama na mtoto na huduma za upasuaji mdogo zitapelekwa” alisema Iddy.

Diwani Bakari Fundikila akiongea na wananchi


Mwanaidi Jamal, mkazi wa Chang’ombe alisema kuwa ujenzi wa Kituo cha Afya Chang’ombe ni suluhisho la tiba kwa wananchi. “Kabla ya kujengwa kwa Kituo cha Afya Chang’ombe ilikuwa lazima kufunga safari kwenda mjini kufuata huduma za afya” alisema Jamal.

MWISHO

 

Comments

Popular Posts

Wananchi Makutupora wafunguka changamoto ya Maji, Umeme na Shule kwa Mkuu wa Mkoa

Waziri Mchengerwa apongeza usimamizi wa miradi jijini Dodoma

Mkataba ujenzi Uwanja wa Mpira wa Miguu wasainiwa Dodoma