Zao la Nyanyachungu na Bilinganya linafaida kwa jamii
Na. Rehema Kiyumbi, DODOMA
Afisa
Kilimo katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Nkunde Kimweri ametoa elimu kuhusiana na zao la
nyanyachungu na bilinganya kwa kuanisha uandaaji, matumizi sahihi ya mbolea na
matumizi ya dawa ya kudhibiti wadudu wanaoathiri zao hilo kwa lengo la kukuza
uchumi kwa wafanyabiashara na matumizi ya nyumbani.
Akizungumza na mwanahabari katika vipando vya Halmashauri ya Jiji la Dodoma alisema kuwa kuna umuhimu mkubwa wa mazao hayo hasa kwa wafanyabiashara. “Tulianza kwa kuandaa shamba la zao la bilinganya aina ya ‘black beauty’ na nyanyachungu aina ya ‘tengeru white’ kwa umbali wa sentimita 60 kwa sentimita 60 ili kuwezesha mmea kuweza kujitanua na kukua kwa uhuru na tulitumia mbolea kutoka Kampuni ya Yara ambapo ni Yara oteshi, na Yara kuzia wakati wa kukuzia mmea wetu na tukatumia dawa viwatilifu kwa kuulia wadudu wanaoshambulia kwa kasi sana zao hili,” alisema Kimweri.
Naye,
msimamizi wa bustani Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Milton Edward alitoa elimu
ya zao la nyanyachungu na bilinganya na kuwashauri vijana wasomi walioko
mitaani wanaochukulia kilimo kuwa ni kazi isiyowafaa. “Niko mbele yenu kuwashauri
vijana wenzangu hasa wasomi ambao wapo mitaani wakisubiri ajira baada ya masomo
yao wajikite katika kilimo ambacho kimegeuka kuwa fursa na kusaidia kujipatia
kipato cha kila siku. Pia, husaidia upatikanaji wa mbogamboga ili kujipunguzia
maradhi yasiyo ya lazima,” alieleza Edward.
Kwa upande wake, Elizabeth Marko mkazi wa machinga ambaye ni mmoja wa watumiaji wa zao la nyanyachungu na bilinganya alieleza jinsi anavyonufaika na zao hili katika matumizi ya familia kama mboga na biashara. “Natumia nyanyachungu na bilinganya kama mboga kwa familia yangu kwa sababu ni mboga rahisi kupika, haziharibiki haraka na ni rahisi kuhifadhi kwenye friji kwa matumizi ya baadae, lakini pia binafsi ninakibanda cha mbogamboga hizi zinazopendwa na watu wengi na ninawauzia kwa bei nzuri kwa ajili ya kuinua kipato changu,” alimalizia Marko.
MWISHO
Comments
Post a Comment