Wapiga kura 795,000 Kugawanywa, Jimbo la Dodoma Mjini
Na. Faraja Mbise, DODOMA
Halmashauri
ya Jiji la Dodoma yawasilisha mapendekezo ya kugawanya Jimbo la Uchaguzi la
Dodoma Mjini lenye jumla ya wapiga kura 795,000 na kuwa majimbo mawili, Jimbo
la Mtumba lenye jumla ya wapiga kura 412,000 na Jimbo la Dodoma Mjini lenye
jumla ya wapiga kura 383,000 kwa lengo la kusogeza huduma karibu na wananchi.
Hayo yalisemwa na Afisa Uchaguzi wa Halmashauri hiyo, Albert Kasoga alipokuwa akiwasilisha taarifa kwa niaba ya Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, ya mapendekezo ya mgawanyo wa Jimbo la Dodoma Mjini, mbele ya Mkutano maalum wa Baraza la Madiwani uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Akizungumza
wakati wa kuwasilisha taarifa hiyo, alisema kuwa mgawanyo huo umezingatia hali
ya kiuchumi ya jimbo husika hasa katika ukusanyaji wa mapato ya ndani sambamba
na kuzingatia ukubwa wa eneo husika.
“Mgawanyo
umezingatia hali ya kiuchumi ya jimbo hasa katika ukusanyaji wa mapato ya ndani
ya jimbo husika. Lengo ni kuona kuwa maeneo yaliyo juu kiuchumi hayamezi
kiuwakilishi maeneo yaliyo chini kiuchumi. Aidha, mgawanyo umezingatia ukubwa
wa eneo ambapo, Jimbo la Dodoma Mjini lilikuwa na jumla ya Kilomita za mraba
2,478.5. Hivyo, mgawanyo katika majimbo mawili umezingatia eneo hilo ambapo
Jimbo la Mtumba lina ukubwa wa kilomita za mraba 1,187.9 na Jimbo la Dodoma
Mjini lina ukubwa wa kilomita za mraba 1,290.6” alisema Kasoga.
Kuhusu
mpangilio wa maeneo ya makazi ya watu na huduma za kijamii zilizopo alisema
mgawanyo umezingatia hilo kwa weledi mkubwa na ili kuhakikisha wananchi
wanasogezewa huduma kwa urahisi.
“Mgawanyo
huu umezingatia mpangilio wa maeneo ya makazi ya watu na huduma za kijamii
zilizopo ndani ya kila jimbo, ambapo Jimbo la Mtumba lina jumla ya kata 20 na
mitaa 99 na Jimbo la Dodoma Mjini lina jumla ya Kata 21 na mitaa 123, huduma za
shule za msingi mgawanyo wake ni shule 59 kwa Jimbo la Mtumba na shule 49 kwa
Jimbo La Dodoma Mjini. Shule za sekondari ni 25 kwa Jimbo la Mtumba na Shule 21
Jimbo la Dodoma Mjini. Vituo vya Afya na Zahanati kwa Jimbo la Mtumba ni
Zahanati 20 na Vituo vya Afya vinne na Jimbo la Dodoma Mjini lina Zahanati 21
na Vituo vya Afya vitano” alisema Kasoga.
Kwa
upande wake, Diwani wa Kata ya Chang’ombe, Bakari Fundikira, alimpongeza Mbunge wa
Jimbo la Dodoma Mjini, Anthony Mavunde, kwa kazi kubwa anayoifanya katika Jimbo
lake na kumtakia heri kwa Mwenyezi Mungu ili azidi kuwatumikia wanachi kwa moyo
wote.
“Tunakupongeza kwa kazi kubwa unazozifanya kwenye jimbo letu, umefanya kazi kubwa sana mheshimiwa Anthony Mavunde, tunakuombea kwa Mungu akubariki na uweze kuwatumikia watanzania wenzetu” alishukuru Fundikira.
MWISHO
Comments
Post a Comment