Mavunde apongeza Baraza la madiwani kupendekeza kugawanywa Jimbo la Dodoma Mjini
Na. Nancy Kivuyo
Mbunge wa Jimbo la Dodoma mjini,
Anthony Mavunde, ametoa pongezi kwa baraza la madiwani kwa kuridhia taarifa ya
mapendekezo ya mgawanyo wa Jimbo la Uchaguzi la Dodoma Mjini kuwa majimbo
mawili.
Katika salamu zake fupi aliishukuru
serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mabadiliko makubwa katika sekta
mbalimbali.
Akizungumzia mgawanyo wa Jimbo la uchaguzi
la Dodoma Mjini na kuwaeleza madiwani faida zitakazopatikana baada ya kugawanya
kwa jimbo hilo. “Jimbo la Dodoma mjini ndilo jimbo kubwa kuliko majimbo yote
hapa nchini likiwa na Tarafa nne, kata 41 na mitaa 222. Nipende kuwaambia,
mgawanyo wa jimbo utaongeza fursa nyingi za kuhudumia wananchi. Mfuko wa jimbo
utasogeza huduma kwa jamii kwa urahisi zaidi, kupitia uwepo wa majimbo mawili,
fedha nzuri itapatikana kwa ajili ya kuboresha miundombinu” alisema Mavunde.
Aliongeza kuwa mipango ya kiserikali
inasaidia huduma za kijimbo kupatikana. Hivyo, kwa majimbo yote mawili watapata
faida kubwa ya kuwa na miradi mingi ya maendeleo katika Halmashauri ya Jiji la
Dodoma. “Naomba niwaambie kuwa, majimbo haya mawili yatatupa faida kubwa sana
na maendeleo ya Jiji la Dodoma yatakua katika viwango vya kipekee” alimaliza
Mavunde.
Wakati akiwasilisha mapendekezo ya
mgawanyo wa Jimbo la Dodoma Mjini, Afisa Uchaguzi wa Halmashauri ya Jiji la
Dodoma, Albert Kasoga alisema “Jimbo la Dodoma Mjini lina jumla ya wapiga kura
795,000 na linatarajiwa kugawanywa katika majimbo mawili. Jimbo moja likiwa na
jumla ya watu 412,000 yaani kata 21 na jimbo lingine lina jumla ya watu 383,000
yaani kata 20. Mgawanyo wa majimbo hayo unazingatia hali ya kichumi ya jimbo,
ukubwa wa eneo, mpangilio wa maeneo ya makazi ya watu na huduma za kijamii
zilizopo kama shule na huduma za afya na upatikanaji wa njia za mawasiliano kwa
maana ya barabara, simu pamoja na vyombo vya habari”.
Katika hatua nyingine, Diwani wa Kata
ya Chahwa, Sospeter Mazengo alisema “napenda kuipongeza Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi
kwa kuweza kutoa fursa kwa majimbo yenye idadi kubwa ya watu kuweza kugawanywa.
Kugawanywa kwa majimbo hayo ni kurahisisha huduma kwa wananchi. Kwa sisi Dodoma
tuna idadi ya watu zaidi ya laki saba, leo tumetumia fursa hiyo na kugawa jimbo
kuwa na majimbo mawili yaani Jimbo la Dodoma mjini litakalo kuwa na kata 21 na Jimbo
la Mtumba litakuwa na kata 20 fursa hii itatusidia sisi wananchi wa Dodoma
kunufaika kutokana na fedha za Mfuko wa Jimbo na kuongeza maendeleo. Hivyo,
naipongeza sana serikali pamoja na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi kwa ajili ya fursa
hio” alisema Mazengo.
Mchakato wa mgawanyo wa Jimbo la
Dodoma Mjini umezingatia masharti ya ibara ya 75 ya Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 ambapo Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ina
mamlaka ya kuchunguza mipaka na kuigawa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika
majimbo ya uchaguzi na kwa kuzingatia masharti ya kanuni ya 18 (1) na (3)
Kanuni za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi za Mwaka 2024.
MWISHO
Comments
Post a Comment