Ujenzi wa Kituo cha Afya Zuzu wafikia 98%
Na. Dennis Gondwe, ZUZU
UJENZI wa Kituo cha Afya Zuzu umefikia asilimia 98 ya
utekelezaji kikitarajiwa kuhudumia wananchi 10,054 kwa kuwahakikishia huduma
bora za afya na kuwaondolea hadha ya kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za afya.
Kauli hiyo ilitolewa na Mwakilishi wa Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Goodluck Magoti alipokuwa akisoma taarifa ya mradi wa ujenzi wa Kituo cha Afya Zuzu kwa Kamati ya Fedha na Utawala ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma ilipofanya ziara ya kutembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho.
Magoti alisema “kutokana na changamoto ya kukosa
huduma za Kituo cha Afya katika Kata ya Zuzu, Halmashauri ya Jiji la Dodoma ilianza
ujenzi wa Kituo cha Afya Zuzu ili kusogeza huduma za matibabu mbalimbali karibu
na wananchi. Halmashauri ilitoa kiasi cha shilingi 299,439,348,54. Hadi kufikia
sasa kiasi cha shilingi 285,4439,000,54 zimetumika kwa ujenzi wa majengo ya Wagonjwa
wa Nje (OPD) na Maabara na kubakiwa na shilingi 14,000,348.54 kwa ajili ya
kuendelea na ujenzi. Ujenzi umefikia asilimia 98 ukiwa katika hatua ya
umaliziaji”.
Akiongelea faida za mradi huo alisema kuwa utakapokamilika
utasaidia watu 10,054 kupata huduma za afya. “Kuwapunguzia akina mama
wajawazito umbali mrefu wa kupata huduma za kujifungua. Kusogeza karibu na
jamii huduma za matibabu ya magonjwa mbalimbali” alisema Magoti.
Kwa upande wa kiongozi wa ‘route’ namba mbili Naibu
Meya, Fadhili Chibago alipongeza na kusema kuwa kazi iliyofanyika ni nzuri. “Niwashauri
kuwa muandae halfa ya uzinduzi wa kituo hiki ili wakazi wa Kata ya Zuzu na
vitongoji vyake wafahamu mchango wa mapato ya ndani ya halmashauri kwa
maendeleo yao ambazo ni kodi zao” alisema Chibago.
Nae Diwani wa Kata ya Miyuji, Beatrice Ngerangera alisema kuwa tukio la uzinduzi wa kituo hicho iwe kumbukumbu ya kihistoria. “Nashauri katika uzinduzi huo uambatane na tukio la kuchangia damu kwa ajili ya kuokoa maisha ya watu. Pia Mheshimiwa Mizengo Pinda ashirikishwe katika tukio hilo kwa sababu ni mkazi wa kata hii” alisema Ngerangera.
Ikumbukwe kuwa Kata
ya Zuzu ilianza kutekeleza mradi wa ujenzi wa Kituo cha Afya tarehe 15 Agosti,
2022 kupitia fedha za mapato ya ndani ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma ukitekelezwa
kupitia mfumo wa ‘force account’ awamu ya kwanza mradi ukihusisha ujenzi wa
jengo la wagonjwa wa nje, maabara na kichomea taka.
MWISHO
Comments
Post a Comment