DC Shekimweri ahimiza usafi kudhibiti magonjwa Dodoma
Na. Shahanazi Subeti, DODOMA
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabir Shekimweri
aliitaka jamii kuzingatia suala la usafi wa mazingira katika maeneo yao ili
kujikinga na magonjwa na kufanya mji kuwa safi na salama katika kipindi hiki
cha maandalizi ya bajeti ya halmashauri ili wananchi wawe na afya bora.
Aliyasema hayo katika Kikao cha Kamati
ya Ushauri ya Wilaya ya Dodoma kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri
ya Jiji la Dodoma kwa ajili ya kupokea na kujadili mapendekezo ya rasimu ya Mpango
na Bajeti ya Halmashauri kwa Mwaka wa fedha 2025/2026.
Alhaji Shekimweri alisema “wenzetu maafisa afya, watendaji wa kata, changamoto za
uchafu wa mji wetu ni usimamizi kwa sehemu fulani, yapo maeneo ya kampuni za
usafi, yapo maeneo yanavikundi vya usafi, lakini ni wajibu wa mwananchi mmoja mmoja
kufanya usafi wa eneo lake. Kwahiyo, tuimarishe usimamizi, na kuna makampuni na
vikundi na vinalipwa kwa kufanya kazi hizo”.
Akiongelea suala la usalama katika
Halmashauri ya Jiji la Dodoma alisema kuwa kamera za usalama (CCTV) ni muhimu
katika kuimarisha usalama. “Tunachokimaanisha
tunapoelekea utaona askari wachache barabarani wanapita kwenye doria, kwasababu
kutakuwa na Kamera zinazofanya kazi, badala ya kutuma askari, watakuwa wanaona
tukio, lakini katika baadhi ya maeneo ya “observation points”
watakaa na pikipiki zao ili kukamata watu wanaofanya matukio ya wizi. Tunataka
tuelekee katika mazingira ambayo hakuna ‘panyaroad’
Dodoma, kwasababu muda wote mji unaangaliwa na mitambo ya kisasa kupitia Jeshi
la Polisi na vyombo vyetu vya ulinzi na usalama” alisema Alhaj Shekimweri.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma alisema kuwa
amepokea mchango unaohusu mkakati wa dharura na majanga. “Mfano
jana kulikuwa na tukio la moto, wengi mmeona fremu takribani 12 na stoo mbili ziliungua
kwa moto lakini tukabaini Jiji letu lina 'fire hydrant’ (mitambo ya kuunganisha kwa ajili ya kuzimia moto) 74 mji
mzima, lakini ambazo zinafanya kazi hazizidi 40. Kwahiyo, Jiji limepokea hiyo
rai kwa haraka kulisaidia Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwasababu wananchi ni wa
halmashauri. Hivyo, ni wa kamati hii ya ushauri wa maendeleo ya wilaya na ndio
walipa kodi. Kwahiyo, ni jambo la wananchi wetu tufanye huduma ya mitambo hiyo” alisema Alhaj Shekimweri.
Aliwataarifu wajumbe kuwa bajeti ya
halmashauri inategemea ukusanyaji wa kodi na kuwataka kudai risiti kwa kila
malipo wanayofanya. “Ndugu zangu wafanyabiashara, wanataka
kuongeza faida, anaweza kukuuzia na asikupatie risiti yeye atapata faida lakini
wewe utakuwa umeidhulumu serikali na umejidhulumu wewe mwenyewe. Maendeleo yote
haya hayawezi kufanyika kama haukusanyi kodi” alisema Alhaj Shekimweri.
Nae, Katibu wa AAFP, Zuhura Mganga, aliishauri
serikali kuhusu Soko la wazi la Machinga kufungwe CCTV kamera za kutosha ili
kuzuia vitendo vya wizi. “Nashauri
kuhusu usalama wa Soko la wazi la Machinga pale kumekuwa na wizi, hakuna kamera
za kutosha na hata kamera zilizopo hazioneshi pande zote” alisema Mganga.
Kwa upande wake Mjumbe wa Halmashauri Kuu
Bakwata, Kakongwe Misambano, alichangia katika suala la afya na usalama
barabarani. “Kwa upande wa afya, ukiangalia tunaongelea
bajeti sana lakini utendaji wake unakuwa hauko sahihi. Mfano, mitaro ya
barabara ya Nkuhungu ambayo imetengenezwa kwa ajili ya bwawa, na linahamisha
watu kila mwaka wakati wa mvua, usalama kwa watoto hakuna kwasababau maji hayaendi
badala yake yanatuwama. Kwahiyo, …bajeti
ambazo zinatengwa zinafanya nini?. Kwasababu, hiyo mitaro inarudisha nyuma,
badala ya kupeleka mbele ili maji yaishe” alisema Misambano.
MWISHO
Comments
Post a Comment