Prof. Mwamfupe; Taka ni fursa ya kutengenezea mbolea
Na. Aisha Haji, DODOMA
Mstahiki Meya wa
Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Prof. Davis Mwamfupe, amewataka wananchi kuendelea
kutunza mazingira na kutumia takataka zinazotokana na mazao kama fursa ya kutengeneza
mbolea ili kuweza kuinua sekta ya kilimo na uchumi wa halmashauri kiujumla.
Aliyasema hayo katika
ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma wakati wa majadiliano na Kamati
ya Ushauri ya Wilaya iliyokutana kupitia mapendekezo ya Mpango na Bajeti ya
Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
Akizungumza kuhusu umuhimu
wa mbolea zitokanazo na takataka za mazao, alisema kuwa taka za mazao ambazo
zinaoza kwa urahisi ni fursa nzuri sana ya kiuchumi kuweza kutengeneza mbolea.
Pia alidokeza kuwa halmashauri imejipanga katika suala la kutoa mikopo, mafunzo
na ushauri wa kitaalamu kwa wananchi kuhusu namna ya kutumia taka zitokanazo na
mazao kwa ajili ya kutengeneza chakula cha kuku kwa kufuata utaratibu maalumu.
Prof. Mwamfupe alisema “halmashauri
itakuwa tayari kupitia taratibu zake za kutoa mikopo lakini vilevile, kutoa
ushauri wa kitaalamu wa namna ya kutumia taka zinazotoka kwenye masoko yetu kwa
ajili ya kutengeneza chakula cha kuku”.
Aidha, aliongeza kuwa wajumbe
wajitokeze katika kuchangia maoni na
ushauri katika kikao cha kamati ya ushauri ya wilaya ili kutambua mambo
mbalimbali yanayowakumba wananchi na kupendekeza masuluhisho. “Ningetamani sana
michango ya watu kama hivi iweze kujitokeza mara kwa mara. Michango hii
tunayoipata hapa tunafurahi kwamba tungekuwa tumepata hata kabla ya wakati huu
kwenye vikao vingine kwa ajili ya kuongelea maslahi ya wananchi” alisema Prof.
Mwamfupe.
Sambamba na hayo
alifafanua kuwa kuna umuhimu wa kuzingatia suala la kupanga bajeti katika mambo
mbalimbali kwasababu bajeti yeyote inaundwa kwa kujumuisha mapato na matumizi. “.....bajeti
inaundwa na hesabu ya makusanyo sawasawa na matumizi yaani kukiwa na senti moja,
senti ishirini imezidi upande mmoja hiyo bajeti imeshindwa” alisema Prof. Mwamfupe.
Vilevile, alitoa rai kwa
wajumbe na wananchi wote kwa ujumla kushirikiana na kuhamasishana katika suala
la kulipa kodi, kukata leseni na kuchangia michango katika vyanzo mbalimbali
vya mapato ili kukamilisha vizuri bajeti ya serikali.
MWISHO
Comments
Post a Comment