Dodoma Jiji U-20 yakita Kambi Kileleni
Na. Mussa Richard, DODOMA
Klabu ya soka ya Dodoma Jiji chini ya umri wa
miaka 20 (U-20) imeendeleza ubabe kwa wapinzani wake wanaoshiriki ligi ya
vijana ya NBC chini ya umri wa miaka 20 Tanzania bara baada ya kuwashushia
kichapo cha mabao 2-1 wanajeshi wa mpakani Mashujaa FC U-20, katika mchezo
uliovulumishwa katika nyasi za dimba la Jamhuri Dodoma hapo jana.
Baada ya mchezo kutamatika kocha wa Dodoma Jiji
U-20, Jeremiah Chido alisema “mchezo umemalizika salama na tumepata kitu
ambacho tulikua tunakihitaji ambacho ni alama tatu muhimu. Alama ambazo
zinatufanya tuendelee kuwa kileleni katika kundi letu na kutufanya tusicheze
kwa presha michezo inayokuja mbele yetu, michezo ambayo tutakuwa ugenini”.
Katika hatua nyingine Chido akaweka wazi
malengo yao kwenye msimu huu wa Ligi ya Vijana ya NBC Tanzania Bara. “Malengo
yetu msimu huu ni kuchukua ubingwa kwasababu msimu uliopita tulifika fainali
ila bahati haikuwa upande wetu. Kwahiyo, msimu huu tukishirikiana halmashauli, mashabikii,
wachezaji na makocha mbalimbali hapa Dodoma nina uhakika tutachukua ubingwa wa Ligi
hii ya vijana kwasababu rasilimali muhimu kwenye mpira ambayo ni wachezaji
tunao na wanaonesha kila nia ya kuhitaji ubingwa” alisema Chido.
Kwa upande wake mchezaji wa Dodoma Jiji U-20,
Christopher Shija ambaye ndiye kinara wa upachikaji mabao mpaka sasa katika ligi
hiyo akiwa na mabao matano baada ya kumalizika kwa mchezo huo alisema malengo
yake ni kuhakikisha anatwaa tuzo ya mfungaji bora wa ligi hiyo.
“Namshukuru Mungu mpaka sasa naongoza
katika orodha ya wafungaji na sijaridhika bado nitaendelea kutumia nafasi kila
nikizipata ili niweze kuwa mfungaji bora. Lakini pia niwashukuru sana wachezaji
wenzangu kwasababu bila wao kunitengenezea nafasi nisingekuwa nafunga. Kwahiyo,
tukiendelea kuwa na ushirikiano ndani na nje ya uwanja tutafanikiwa katika
malengo yetu kama timu na mchezaji mmoja mmoja” alisema Shija.
Baada ya ushindi huo Dodoma Jiji U-20
imefanikiwa kukusanya alama 22 kibindoni ikishuka dimbani katika michezo tisa
ikibakisha michezo mitano kumaliza hatua ya makundi, huku ikiendelea kushika
usukani katika kundi A. Katika michezo iliyosalia Dodoma Jiji U-20 inahitaji
walau alama mbili ili kujihakikishia kufuzu hatua ya robo fainali ya ligi hiyo
ambayo inachezwa katika mfumo wa makundi mawili ambapo nafasi ya kwanza hadi ya
nne kwa kila kundi moja kwa moja zinatinga katika hatua ya robo fainali.
MWISHO
Comments
Post a Comment