Timu ya Pete ya Combine yatubu kwa Timu ya Elimu Msingi
Na. Coletha Charles, DODOMA
Timu ya Mpira wa Pete
ya Elimu Msingi imeibuka na ushindi wa kishindo kwa kuifunga Timu ya Combine (Elimu
Sekondari na Watendaji wa kata) kwa mabao 9-5 ambapo mchezo huo ulifanyika
kwenye uwanja wa Jamhuri, ukiwa na ushindani mkubwa huku kila upande ukionesha
mchezo wa hali ya juu.
Mchezo ulianza kwa
kasi huku Timu ya Elimu Msingi ikiongoza katika robo ya kwanza kwa mabao 4-1 wakitumia
uzoefu wa wachezaji wao wakongwe. Hata hivyo, Combine walionesha nidhamu ya
hali ya juu na kutumia mbinu bora za kiufundi, katika robo ya pili timu zote
ziliongeza kasi ili kupata alama muhimu za ushindi huo wa kihistoria.
Kocha wa timu ya
Elimu Msingi, Emma Ernest, alisema kuwa, walishinda kwa sababu nyumba bila msingi
hauwezi kujenga. Hivyo, waliweka msingi imara ndio maana waliweza kushinda kwa
kishindo kwa kufanya mazoezi. “Tulijiandaa vya kutosha kwa mchezo huu.
Wachezaji wangu wameonyesha nidhamu, umoja, na uwezo wa kupambana hadi dakika
ya mwisho. Ushindi huu ni wa juhudi za pamoja. Tulijua kuwa mchezo utakuwa
mgumu, lakini tuliweka mikakati ya kimpira na kisaikolojia ambayo iliwasaidia
wachezaji wetu kuwa imara. Ushindi huu ni muhimu kwetu na tunajivunia mafanikio
haya” alisema Ernest.
Kwa upande wake,
Kocha wa Combine, Theopister Andrea, alikiri kuwa timu pinzani ilikuwa bora
zaidi katika mchezo na timu yake ilikosa umakini katika upande wa wafungaji,
lakini aliahidi atafanya marekebisho. “Tulijaribu kadri ya uwezo wetu, lakini
Timu ya Elimu Msingi walikuwa na mpango mzuri wa mchezo. Tumepoteza nafasi
muhimu ambazo zilitugharimu, lakini tutajitahidi kufanya mazoezi ya ziada ili
tuwe bora zaidi katika michuano” alisema Andrea.
Nae, Nahodha wa
Timu ya Elimu Msingi, Jane Thawe, alisema ushindi huo ulikuwa matokeo ya
maandalizi mazuri na mshikamano wa timu na walijipanga kwa ajili ya mashindano
haya. “Tulijitahidi sana, hasa katika robo ya mwisho. Ninamshukuru kila
mchezaji kwa juhudi zake, Timu ya Combine wakati mwingine wajipange na sisi
tunakikosi kipana kilichoingia leo ni kikosi ‘C’ tu na tulikuwa tunafanya
mazoezi usiku na mchana kwa hiyo ushindi ni kawaida yetu” alisema Thawe.
Aidha, Nahodha wa
Timu ya Combine, Evarista Mkalawa, alikubali matokeo kwa moyo wa sportsmanship na kuwapongeza wapinzani
wao. “Walistahili kushinda, lakini tumejifunza mengi kutoka kwenye mchezo huu,
tulizidiwa nguvu na wenzetu lakini tuko vizuri na katika mchezo ukifanya kosa
moja mpinzani anatumia nafasi hiyo kukuadhibu, tumekubali tumeshindwa.
Tunaahidi kurejea tukiwa imara zaidi” alisema Mkalawa.
MWISHO
Comments
Post a Comment