Na. Coletha Charles, DODOMA
Muelimishaji wa Darasa Tembezi Halmashauri ya Jiji la Dodoma,
Chacha Marwa amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura ifikapo tarehe
27 Novemba, 2024 katika vituo husika.
Marwa alitoa elimu hiyo kwa wananchi waliopanda gari tembezi
kutoka Soko la wazi la Machinga hadi Hospitali ya Benjamin Mkapa kwa kuwakumbusha
kuwa haki ya kiongozi bora ipo mikononi mwao.
Alisisitiza kuwa kupiga kura ni msingi wa maendeleo katika
mitaa yao kwa kuzingatia haki na kutokupokea rushwa ya aina yoyote kutoka kwa
wagombea wa nafasi ya mwenyekiti na wajumbe watano (5) wa serikali za mitaa.
“Elimu hii ni muhimu kwa wananchi wote hasa mliojiandikisha
kwenye orodha ya daftari la wapiga kura, ni muhimu sana kupata haki yako ya
msingi, msipoenda kupiga kura mtashindwa kupata viongozi bora wa kuleta
maendeleo. Mjitahidi kuchagua viongozi wazalendo wenye busara kwa kusikiliza
sera zao. Pia walemavu ambao hawezi kufika katika vituo vya kupiga kura, serikali
inashauri wananchi kuwafikisha katika vituo ili waweze kupiga kura kwasababu ni
haki yako” alisema Marwa.
Aidha, Serikali imetenga rasmi tarehe 27 Novemba, 2024 kuwa
siku ya mapumziko kwa wafanyakazi na watu wote ambapo zoezi la kupiga kura
litaanza saa 02:00 asubuhi hadi saa 10:00 jioni.
MWISHO
Comments
Post a Comment