Jiji la Dodoma lasaini mkataba ujenzi wa barabara ya lami kwenda Hospitali ya Jiji
Na. John Malima, DODOMA
Halmashauri ya Jiji la Dodoma imesaini
mkataba wa makubaliano ya ujenzi wa barabara kutoka Hospitali ya Halmashauri ya
Jiji la Dodoma hadi barabara kuu ya Singida yenye urefu wa Kilomita 1.6 kwa
kiwango cha lami.
Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma, Prof. Davis Mwamfupe (kustoto) na Mkurugenzi wa Jiji, Dkt. Frederick Sagamiko wakisaini mkataba wa ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami
Mkataba huo ulisainiwa tarehe 20 Novemba,
2024 katika Ofisi ya Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma baina ya
Halmashauri ya Jiji la Dodoma na Kampuni ya ujenzi ya Kings Builders Limited
ukiwa na thamani ya shilingi 2,431,050,561.63 (Bilioni Mbili na Milioni Mia Nne
Thelathini na Moja Laki Tano na Mia Tatu Sitini na Moja na senti Sitini na Tatu).
Katika zoezi la kusaini mkataba huo
Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Prof. Davis Mwamfupe alimshukuru
Mkandarasi kwa kuunga juhudi za serikali na alimtaka kufanya kazi kwa viwango
vinavyotakiwa. “Kwanza nawapongeza sana, mmetimiza adhma ya serikali kwamba katika
miradi iliyo mingi tunasisitiza sekta binafsi, lakini tungependa msiwe vikwazo katika
utekelezaji wa miradi yenu kwasababu Dodoma ni makao makuu ya nchi. Kama
utendaji kazi wenu utakuwa wa viwango, mtakua mnaunga mkono juhudi za serikali.
Kwahiyo, lazima tuhakikishe ubora wa miundombinu ili kuifanya sekta ya afya
istawi zaidi” alisema Prof. Mwamfupe.
Kutokana na changamoto mbalimbali za
wakandarasi kutokumaliza miradi yao kwa wakati, Mstahiki Meya alimtaka mkandarasi
kutokuwa kero katika utekelezaji wa mradi huo kwa visingizio mbalimbali. “Tungependa
ninyi msije mkawa kero, kwa maana kwamba kazi zenu haziishi kwa visingizio
visivyoisha kama vifaa, bei na vingine vingi, hatutegemei kujuta kutokana na kazi
hii kwasababu ubora wa kazi hii ni namna ya kuomba kazi nyingine tena”
alisisitiza Prof. Mwamfupe.
Mkandarasi Eng. Joseph Tarimo (kulia) akisaini mkataba wa ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami
Kwa upande wake, Mkandarasi wa Kampuni ya Ujenzi
ya Kings Builders Limited, Mhandisi Joseph Tarimo, aliyesaini mkataba huo
amesema watajitahidi kufanya kazi kwa muda walioahidi wakizingatia ubora katika
mradi huo.
“Sisi kama kampuni, tunaunga mkono yale
aliyosema Mstahiki Meya, kampuni tutafanya kazi usiku na mchana kuhakikisha
kuwa tunakamilisha kazi ndani ya muda wa mwaka mmoja lakini ni mategemeo yetu
tutafanya kazi hii kwa pungufu ya muda uliopo katika mkataba wetu” alisema”
Mhandisi Tarimo.
Ukarabati wa barabara hiyo kwa kiwango cha
lami utakuwa na manufaa kwa wakazi wote wa Jiji la Dodoma kwasababu
itarahisisha upatikanaji wa huduma ya Afya na shughuli za uchukuzi.
MWISHO
Comments
Post a Comment