Kura Yako Maendeleo ya Mtaa
Na. Coletha Charles, DODOMA
Timu hamasa ya
Halmashauri ya Jiji la Dodoma, imeendelea na zoezi la kuwahamasisha wananchi
kushiriki kikamilifu katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa katika maeneo
mbalimbali ya halmashauri hiyo.
Zoezi hilo lilifanyika
katika eneo la Soko la wazi la Machinga hadi Ihumwa kwa lengo la kuwakumbusha
na kuwasisitiza wananchi umuhimu wa kupiga kura kwasababu ni msingi mzuri wa
kuleta maendeleo katika mitaa yao.
Muelimishaji wa katika
gari maalum lijulikanalo kama darasa tembezi, Isabella Bruno alisema kuwa
kupitia Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Dodoma kwa kushirikiana na Mkurugenzi wa
Jiji la Dodoma, wametoa gari la darasa tembezi kwa lengo la kuhamasisha
wananchi kushiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka huu.
Alisema kuwa wananchi
wanatakiwa kuchagua viongozi wenye sifa kwa kusikiliza sera zao kipindi ambacho
kampeni zitakapoanza tarehe 20 Novemba, 2024 na kuangalia kiongozi wa
kuwaongoza kwa muda wa miaka mitano ya uongozi.
“Tunafanya hivi
kukupa uelewa wewe mwananchi na kukukumbusha kuwa ni wajibu wako kupiga kura,
kama tunavyofahamu wananchi wengi tumekuwa na kasumba ya kutokushiriki masuala
ya uchaguzi kwa sababu mbalimbali na wengine wanakuwa hawaoni umuhimu wa
kushiriki” alisema Bruno.
Kuhusu suala la rushwa,
wananchi wametakiwa kutojishughulisha na kutoa au kupokea rushwa kwa lengo la
kumchangua kiongozi asiye sahihi kwasababu uchanguzi huu ni wa amani na
wakuleta tija katika nyanja tofauti tofauti.
Uchaguzi huu unatarajiwa
kufanyika tarehe 27 Novemba, 2024 na kila mwananchi mwenye sifa na vigezo vya kushiriki
atatakiwa kupiga kura akiwa ni mtanzania halisi, mwenye umri kuanzia miaka 18
na kuendelea, mwenye akili timamu, mkazi wa mtaa husika na awe amejiandikisha
kwenye orodha ya daftari la wapiga kura.
MWISHO
Comments
Post a Comment