CCM yampongeza Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan utekelezaji Ilani

Na. Dennis Gondwe, DODOMA

CHAMA cha Mapinduzi (CCM) kimempongeza Rais, wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi katika sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.



Pongezi hizo zilitolewa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Tanzania Bara, John Mongela alipotoa salamu za CCM katika kilele cha maonesho ya Nanenane kitaifa, Nzuguni Dodoma.

Mongela alisema “Ilani ya CCM ina kurasa 308, kurasa 33-56 zinaelezea sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi. Leo mimi ni shahidi kwamba utekelezaji wa Ilani unafanywa kwa kiwango cha juu sana, tumpongeze Rais na serikali yake. Chini ya uongozi wako ni kazi kubwa inatambulika kwenye sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi”.

Aidha, aliahidi CCM kuendelea kufanya kazi karibu na serikali ili wananchi wapate maendeleo zaidi.

Akitoa salamu kutoka kwa mabalozi wa nchi za nje, Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Michael Battle alisema kuwa washirika wa maendeleo wanaunga mkono juhudi za Tanzania katika kukuza sekta za Kilimo, Mifugo na Uvuvi hasa ushiriki wa wanawake na vijana.

Alisema kuwa Serikali ya Marekani itaendelea kuchangia katika Kilimo cha Tanzania kupitia mpango wa Feed the Future unaofadhiliwa na USAID.

Aidha, alimhakikishia Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa Marekani na washirika wake wapo tayari kuitangaza Tanzania kuwa imefunguka kibiashara. “Mungu akupe nguvu na hekima ya kuongoza Tanzania” alimalizia Balozi Battle.

Maonesho ya Nanenane mwaka 2024 yanaongozwa na kaulimbiu isemayo “Chagua viongozi bora wa serikali za mitaa kwa maendeleo endelevu ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi”.

MWISHO

 

Comments

Popular Posts

Wananchi Makutupora wafunguka changamoto ya Maji, Umeme na Shule kwa Mkuu wa Mkoa

Waziri Mchengerwa apongeza usimamizi wa miradi jijini Dodoma

Mkataba ujenzi Uwanja wa Mpira wa Miguu wasainiwa Dodoma