Wizara yatakiwa kutoa msaada wa kisheria kwa wananchi

Na. Josephina Kayugwa, DODOMA

Wizara ya Katiba na Sheria yatakiwa kutekeleza kikamilifu msaada wa kisheria kwa wananchi kwa lengo la kutenda haki.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan akiongea na mamia ya wanasheria na wananchi


Hayo yalisemwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan katika maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini yaliyofanyika katika bustani ya mapumziko ya Chinangali yakiongozwa na kaulimbiu inayosema ‘Umuhimu wa dhana ya haki kwa ustawi wa Taifa, Nafasi ya Mahakama na wadau katika kuboresha Mfumo Jumuishi wa Haki Jinai’.

Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan alisema taasisi zote za kisheria zinatakiwa kushirikiana katika jambo la kutenda haki kwa jamii na kuimarisha mfumo wa haki hii ni kutokana na kucheleweshwa na mashauri ambayo yanatakiwa kutekelezwa mapema.

“Muda wa mashauri ya kimahakama unatakiwa kupunguzwa ili kuwapa nafasi wananchi kwaajili ya kuendelea kutekeleza mambo mengine ya kimaendeleo na majaji wote mnatakiwa kutokutoa hukumu za dhuluma. Na niwapongeza kwa kuwa na kuanza mwaka mpya wa Mahakama na kuwa na mfumo sahihi utakaowezesha kupunguza mashauri ya kesi mahakamani” alisema Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Kwa upande wake Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji. Dkt. Eliezer Feleshi alisema viongozi wa serikali wanatakiwa kuzingatia miongozo ya kisheria iliyotolewa katika kutatua migogogro mbalimbali inayowakumba wananchi.

“Ofisi yangu kama Mwanasheria Mkuu wa Serikali ipo wazi kwa viongozi na wananchi kwaajili ya kupata masaada wa kisheria pamoja na elimu juu ya sheria na haki” alisema Jaji. Dkt. Feleshi.

Sambamba na hilo Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika, Aloyce Sungusia alimpongeza Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweka kipaumbele katika mfumo wa haki jinai.

Alisema lengo la maadhimisho ya Siku ya Sheria ni kuboresha mahusiano mazuri kwa wadau wa sheria, kutoa huduma ya msaada wa kisheria kwa wananchi kutoa elimu ya haki jinai kwa umma.

“Tutaendelea kuhimiza utendaji haki kwa kila mwananchi ikiwemo kuwapa elimu kuhusu sheria na haki jinai na kuisaidia Serikali, Bunge na Mahakama” alisema Sungusia.

Maadhimisho ya Siku ya Sheria hufanyika Februari 1 ya kila mwaka.



MWISHO

Comments

Popular Posts

Jiji la Dodoma lapewa angalizo lishe bora kwa wananchi

RC Dodoma apongeza wafugaji kwa ushiriki wa Paredi ya Mifugo

Rais Samia: Tumieni kikamilifu Miundombinu, Teknolojia na mitaji iliyowekezwa katika Kilimo, Uvuvi na Mifugo