TIMU YA WATUMISHI JIJI LA DODOMA YAIBUKA KIDEDEA KWA KUBEBA VIKOMBE 5 SHIMISEMITA TAIFA
Na. Dennis Gondwe, DODOMA
TIMU
ya Watumishi ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma iliyoshiriki michezo ya
Shirikisho la Michezo Serikali za Mitaa (Shimisemita) ilikuwa tishio kwa
kushinda michezo yote mpaka fainali na kuzoe vikombe vitano.
Katibu wa Timu ya Watumishi Jiji la Dodoma, Emma Ernest alipokuwa akisoma taarifa fupi ya michezo ya Shimisemita
Kauli hiyo ilitolewa na Katibu wa Timu ya Watumishi Jiji la Dodoma, Emma Ernest
alipokuwa akisoma taarifa fupi ya michezo ya Shimisemita ngazi ya taifa mwaka
2023 kwa Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma katika hafla fupi ya kukabidhi vikombe walivyoshinda
katika mashindano ya michezo ya Shimisemita katika ukumbi wa mikutano wa jiji
hilo.
Ernest
alisema “katika michezo yote timu yetu ilikua ni tishio katika mashindano
kwasababu michezo yote tuliyocheza hatukuwahi kufungwa hata mechi moja,
tulishinda mechi zote kutoka hatua ya mzunguko mpaka fainali. Timu ya mpira wa miguu ndiyo iliishia robo
fainali kwa kutolewa na timu ya Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba kutokana na
wachezaji wengi kuwa majeruhi”.
Alisema
kuwa katika mashindano hayo halmashauri hiyo iliweza kushiriki michezo yote
pamoja na changamoto ya uchache wa wachezaji. “Wachezaji walijituma kwa moyo
wote na kuweza kushinda michezo yote na Jiji la Dodoma kuibuka kidedea mshindi
wa jumla kwenye michezo ya Shimisemita mwaka 2023 na kuipeperusha bendera ya
Jiji la Dodoma ipasavyo. Pamoja na hayo Daktari Bora wa mashindano aliyeokoa
maisha ya wachezaji wote alitoka katika halmashauri yetu ambae ni Dr. Baraka F.
Edwin” alisema Ernest.
Timu
ya watumishi wa Jiji la Dodoma ilishiriki michezo ya mpira wa miguu, mpira wa
pete, mpira wa wavu, mpira wa mikono, pooltable, draft, darts, ngoma, karata na
riadha. “Ikiwa na jumla ya wachezaji 40, Daktari 2, Kocha 2, Dereva, Timu
Meneja, Katibu, Mwenyekiti, Afisa utumishi na Mlezi wa Timu. Tunamshukuru
Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma kwa juhudi na jitihada alizozionesha kwa wachezaji
kwa kuwatia moyo na kuwawezesha kushiriki mashindano tukiwa na afya njema,
tabasamu la ushindi lililopelekea kurudi na ushindi mnono huku tukiziangusha
Halmashauri 69, tunakupongeza sana mwajiri wetu na tunaimani na wewe uzidi
kututia moyo ili bendera ya Jiji la Dodoma ipepee kwa shagwe kwa kila sekta
ndani na nje ya nchi yetu” alisema Ernest.
Mashindano
ya Shimisemita yalianza tarehe 18-30 Oktoba, 2023 na timu ya watumishi wa
Dodoma Jiji iliibuka mshindi wa jumla kwa kunyakua makombe matano, wanawake
nafasi ya mshindi wa kwanza katika mpira wa pete, wavu, na mikono, huku wanaume
wakishika nafasi ya pili mpira wa mikono na medali nne (mbili pooltable, moja
draft na moja kurusha tufe) huku daktari bora wa mashindano aliyeokoa maisha ya
wachezaji wote alitoka Jiji la Dodoma.
MWISHO
Comments
Post a Comment